DOMO KAYA: Ama kweli yote ni vanity!

DOMO KAYA: Ama kweli yote ni vanity!

Na MWANAMIPASHO

MIMI sio mshauri nasaha, wala mtaalamu wa ndoa ila nimewahi kuwa kwenye ndoa lakini haikusimama.

Mwaka wa kwanza na nusu niliamini kuwa nimepata jembe, kumbe baba nilikuwa nimepatikana.

Miaka mitatu baadaye ndoa ikavunjika na mtoto wa watu nikajitoa.

Mara si moja nimesikia wanaume wakilaumiwa kwa kuvunja ndoa zao. Sipo hapa kuwatetea ila hata na wanawake ni wa kulaumiwa.

Sina uhakika na yaliyojiri katika ndoa ya Daddy Owen na mke wake Farida Wambui ila kama ni kweli, nimemsikitikia sana mwanamuziki huyo.

Mr Vanity alimwoa mtoto wa watu Farida Wambui miaka mitano iliyopita na wakaishia kujaaliwa watoto wawili. Kwenye Instagtram yake, Owen aliishi kumsifia sana mkewe kila uchao. Ilikuwa kawaida kwake kutupia picha zao wakila maisha ungedhani hawakuwa wakikosana. Juzi ikaibuka taarifa kwamba mkewe aliondoka akimtaarifu kwamba anasafiri kwenda Gilgil kwa shughuli ya kibiashara.

Mtoto wa watu ndivyo alivyoenda mazima na mpaka sasa hajarudi. Stori ni kwamba Farida alikuwa akimchepukia kimya kimya Owen na bwanyenye mmoja kwa jina Njuguna aishiye huko Gilgil. Ndiko huko alikoishia Farida na kumwacha Owen kwa mataa. Stori zilipoanza kuzagaa, Owen akathibitisha kabisa kwamba mambo sio sawa kwa kufuta picha zote alizokuwa ameposti za mkewe kwenye Instagram.

Wapo waliohoji kwamba anatumia skendo hiyo kama kiki ili kusukuma wimbo wake mpya. Kusema kweli hili mimi halikuniingia kichwani toka mwanzo. Kwa miaka yote hiyo aliyofanya muziki, ameachia hiti bila ya kutumia kiki, iweje sasa.

Juzi kati pia alitoa taarifa akiwashukuru waliomfariji na kumpigia simu kumtia moyo. Hakuthibitisha wala kukana kuachwa ishara tosha kwamba kweli ndoa yake imeingia mdudu.

Nilipo ninajua uchungu anaopitia Owen, naamini kabisa kwamba katika hili anapitia kipindi kigumu tena sana. Mkeo wa ndoa kukukimbia tena akaishia kwa mikono ya tajiri, hii inakuambia nini? Huu ni udhalilishaji mkubwa kwa mwanamume yeyote na huuma hata kuliko usaha.

Tetesi zinadai kuwa kabla hajagura na kumwacha kwa mataa, siku za hivi karibu Owen na mkewe waliishi kugombana sana. Ila pamoja na ugomvi wote Owen anasemekana mara si moja alikuwa akijitahidi kumbembeleza mkewe angalau waweze kuiokoa ndoa yao ila ni kama mtoto wa watu alikuwa tayari ashaipata spea-tairi. Lakini pia mtoto wa watu anasemekana anatokea familia yenye pesa hivyo maisha ya msoto hawezi kuvumilia.Tetesi zinadai kuwa chanzo kikubwa cha kuvunjika kwa ndoa yake Owen ilikuwa Covid. Janga la Covid lilipogonga, lilifunga mifereji yote ya pesa kwa watumbuizaji. Owen kama wasanii wenzake akakosa shoo za kumwigizia kipato.

Maisha yakaanza kuwa magumu na hapo ndipo mkewe Farida anadaiwa kubadilika na kuanza kuonekana viwanja tofauti akiwa na watu wenye pesa na nafasi zao.

Mishe mishe za mkewe zikaongezeka maradufu na Owen akaanza kupokea ripoti mbalimbali za kuwa mkewe kaonekana maeneo tofauti tofauti ya kifahari. Hii ikawa ndio chanzo cha ugomvi wao wa mara kwa mara. Ila pamoja na ugomvi, Owen alijitahidi sana kuiokoa ndoa yake. Lakini watu wake wa karibu wanasema hali mbaya ya kifedha haingemruhusu huku mtoto wa watu akiwa tayari ameshapata mbadala.

Madai haya yananikumbushia kabisa ndoa yangu. Visanga vilikuwa kama hivi tu. Ndio maana daima nachukia msoto lakini pia nimeishi kuwa makini sana na wanawake waliofuata baadaye. Viumbe hawa huwalaumu sana wanaume lakini pia wao wanashawishika haraka.

Kuvunjika kwa ndoa yangu na hii ya Owen kulinifunza mambo kadhaa. Mwanzo kabisa wanawake wengi walioachika na ukawakuta wana wana, kuwa makini kuelekwa kiini cha kwa nini ndoa au mahusiano yao ya awali hayakutoboa.

Mwogope mwanamke anayetokea familia ya kitajiri ikiwa na wewe hupo katika levo hizo. Mapenzi yanaweza kuwanogea ila msoto utakapobisha ukashindwa kuokoa hali, basi ndio mwana utajua mbivu na mbichi. Najua umeshawahi kuona misemo kwenye kanga ‘Filisika ujue tabia za mkeo’. Ndio mambo haya sasa.

Kama wewe ni staa kama alivyo Owen, kuwa makini na hawa mademu, jitahidi kumpata mwanamke anayekuthamini na wala sio anayetaka kuwa na wewe kwa sababu ya umaarufu wako. Ni mtazamo tu.

You can share this post!

Wizi wa mifugo wazidi kijijini Ngoingwa

‘Msoto’ watisha kuyumbisha Gor mwaka mpya ‘21