Makala

DOMO KAYA: Hekaya za Zari na Diamond

July 26th, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

AISEE! Nikuambie kitu?

Kama kuna suala moja ambalo limenishinda kufuatilia kabisa ni hivi visanga vya Diamond na mpenzi wake wa zamani Zari Hassan.

Hawa watu buana hata baada ya kuachana mwaka mmoja uliopita bado wanavuruga sana utadhani kuwa bado wapo pamoja.

Miezi michache iliyopita takriban minne hivi, Diamond alitokea kwenye mahojiano na redio yake Wasafi FM na kumshtumu Zari kwa kumkazia kuwacheki watoto wake.

Pia alisema alikuwa anatuma pesa za matumizi takriban laki 200,000 kila mwezi ila ilifikia kipindi akaacha kwa sababu ya kukaziwa watoto.

Kuhusu michepuko yake, alijitetea kwa kusema alianza baada ya kugundua Zari alikuwa akimchepukia na mwalimu wake wa mazoezi.

Lakini buana ni nani asiyemjua Diamond na tabia zake za uzinzi?

Hapo kumwamini nilishindwa. Ila hata zaidi, huyo mwalimu wake Zari wa mazoezi kama ulimcheki, mbona anao mvuto sana kumliko Diamond!

Kama ilitokea, naweza kushindwa kumlaumu Zari ukizingatia kwamba walikuwa wanaishi mbali. Mmoja yupo Sauzi mwenzake Dar.

Baada ya Diamond kumwaga yake, wiki iliyopita Zari alipata fursa naye kufunguka kupitia Ayo TV iliyosafiri hadi Sauzi kumsikiza. Hakika bibiye alifunguka mengi.

Kuanzia kwa Diamond kupiga mnada mjengo aliomununulia kwa ajili ya watoto wake, uongo wake kwenye suala la kutuma pesa za matumizi na hata kulenga kuzungumza na wanawe kwa zaidi ya miezi tisa.

Ukizisikiza hekaya za Diamond kisha uambatanishe na mipasho ya Zari, unaweza ukachanganyikiwa ushindwe nani mkweli hapa.

Ila kwa upande wangu sijui kwa nini nahisi kumwamini zaidi Zari kumliko huyu Mondi. Nafikiri kwa sababu huyu jomba ni mwongo tena hajui kuficha uwongo. Ila sio kusema kwamba hana ukweli wake jamani.

Lakini yote tisa hayo hayanihusu. Mimi kile kikubwa nilichoshika kutoka kwa mahojiano ya Zari ni ule wosia aliomrushia Tanasha kuhusu ujauzito alionao ambaye kwa sasa anadekezwa we acha tu.

Kufyonza mafuta

Kwenye sherehe ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa tarehe saba mwezi huu wa saba, mtoto wa watu alifanyiwa bonge la pati na hata kukabidhiwa gari jipya aina ya Toyota V8.

Mwanangu kama huna hela za kutosha kugharimia mafuta, huu mkebe wala usiuwazie hata kwenye ndoto zako.

Shamrashara alizofanyiwa Tanasha zinatosha kumfanya mwanamke yeyote hata hawara kuhisi kudhaminiwa. Ila Zari alikuwa makini kumwonya kwamba vimbwanga hivyo visimfanye kipofu. Aishi kwa kufahamu kuwa Diamond hatabiriki. Mwenyewe mara nyingi kasema hatabiriki. Hii ikiwa na maana kuwa, hata ujauzito huo haitakuwa ajabu akijikuta akimlea mtoto huyo mweyewe.

Alichomchanua Tanasha nacho ni kwamba aanze mapema kujijengea fikra za kumlea mtoto wake solo endapo Diamond ataamua kuanza kumpiga na matukio. Wanasema mwenye macho haambiwi tazama.

Zari alimpa mifano ya yeye na EX wengine waliotangulia kama funzo. Hakika kama Tanasha atapuuza nasaha hiyo, basi atakuwa ni mpumbavu wa mwisho. Amwangalie Zari alivyoachanishwa, Hamisa Mobetto, Wema Sepetu sema kwa bahati mbaya au nzuri hakuachwa na mtoto, na mademu wengine kibao aliovuka nao Diamond. Mapenzi yanalewesha ila katika hili, bora Tanasha anywe juisi.