Makala

DOMO KAYA: ‘Kakinuka, acha kanuke’

October 9th, 2020 2 min read

Na MWANAMIPASHO

STORI inayotrendi kwa sasa inahusu ndoa yake mwanamuziki wa injili Size 8 Reborn na mume wake DJ Moh.

Stori ni kwamba kamchepukia mke wake na sasa kimenuka. DJ Moh ni miongoni mwa wasanii ambao hujigamba mitandaoni kuwa watakatifu na wanavyoelewa mafundisho ya Biblia hata kuwaliko mapasta.

Ni kwa misingi hii ndiyo sababu alipewa fursa ya kuwa nahodha wa kipindi cha injili Crossover 101 pale NTV.

Sasa sijui skendo hii ambapo kaanikwa na bloga Edgar Obare kwa kumchepukia mke wake, kama itamharibia kazi NTV. Heshima yake sasa lazima itashuka. Nani atamwamini kuwasilisha kipindi cha injili?

Kuna binti mwenye tabia za usoshiolaiti ambaye kamwaga ushahidi wa kutosha kusapoti madai yake kwamba amekuwa akichepuka naye. Aisee! Hata mimi nimemwamini. Kuna kila sababu za kuamini madai ya binti huyo. Hadi katoa ushahidi wakipiga ‘video call’. Suala la DJ Moh kumchepukia Size 8 limekuwepo kwa muda sasa. Msupa huyu alishawahi toroka nyumbani kwao na kwenda kukodisha kwingine kwa sababu ya tabia hii. Alimsamehe mumewe wakarudiana.

Kilichonisinya sana ni kumsikia binti huyo akidai kwamba DJ Moh alikuwa akimtoa rangi mkewe kuhusu kiwango cha mchezo wake chumbani. Hii ndio sababu amekuwa akimchepukia eti. Alidai kwenye masuala ya kitandani, eti mwanamama hajui kujiongeza. Au pengine ndiyo sababu alichoma zile tisheti zake za ‘seng’enge ni ng’ombe?’. Nawaza tu.

Nimemshukishia heshima huyu jomba. Unawezaje kumwongea vibaya mwanamke ambaye upo kwenye ndoa naye tena kwa miaka sita, hata kama unayoyasema ni kweli? Huyu ni mama wa watoto wako wawili. Huyu ni mwanamke alikuja katika maisha yako na kukusaidia kukua. Huyu ni mwanamke ambaye kakusaidia kuongeza umaarufu wako. Nyie kama familia mkiwa kitu kimoja mumefanikiwa kupata dili kibao za matangazo. Jamani hata kama sio mtamu kama unavyodai, sioni sababu za kwenda kumwanika kule nje. Kule ni kumdhalilisha lakini kubwa zaidi unajidharau mwenyewe. Unachepuka mpaka hujali.

Kila nikimsikiza DJ Moh anachomlaumia mkewe, ni kwamba dada huyu ana kidomodomo na kuwa ni chiriku. Nafahamu Kabisa wanaume wengi nikiwemo hatupendi wanawake wenye mdomo mkali au mwanamke apendaye kelele. Lakini jamani kipindi wanaanzisha mahusiano alikifahamu hiki kuhusu Size 8 na bado akamkubali tu.

Isitoshe, ni kwa nini Size 8 asipige kelele wakati akiwa anajua vyema aina ya mume aliyenaye nyumbani! Mwanaume anayejifanya kuheshimu ndoa na kumwogopa Mungu ila akiamua kuchepuka, atampigia simu mke wake akiwa ameondoka nyumbani kumfahamisha kwamba hatakuwa akirejea nyumbani kwa wiki nzima kwa sababu kapatwa na kazi ya dharura. Sasa mke wake akianza kuja juu, anaanza kumgeuzia kwa kudai mwenzake anapenda kelele.

Namhurumia Size 8 alipo sasa hivi. Machungu anayopitia. Ila nitakwambia kitu kimoja, mimi sio mtaalamu wa ndoa na mapenzi lakini ninachojua ni kuwa msingi wa ndoa hii ya Size 8 na DJ Moh ilijengwa vibaya. Miaka sita iliyopita Size 8 alikuwa msanii wa muziki wa ‘secular’. Alikuwa ni maarufu sana. Ghafla tukasikia kaokoka. Kumbe ni baada ya kukutana na DJ Mo wakapendana na akashawishika kubadili muziki wake.

Kisha kilichofuata ni ndoa ya chini ya maji. Hatujawahi kuona picha hata moja ya harusi yao licha ya kuendelea kusisitiza kuwa walioana kimya kimya. Wapelelezi wangu wameshanifahamisha kuwa hawa walifunga ndoa kwenye afisi za AG. Ndoa ya Kikristo ikafungiwa kwenye afisi ya mwanasheria mkuu? Sasa leo ikiwa imepata nyufa, sioni cha kushangaza hapa. Ila kuhusu hilo la Dj Moh kuchepuka, ilikuwa ni bomu iliyokuwa inasubiri muda ilipuke. Kwa maneno yake DJ Moh, nitaaga kwa kusema ‘Kama kakinuka, acha kanuke’!