Makala

DOMO KAYA: 'Kalikuwa katoto hodari’!

September 20th, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

KUNA jambo limenisikitisha sana.

Wiki iliyopita mwanamuziki wa WCB Mbosso Khan alikutwa na msiba.

Ule msiba aliokuwa nao ulihusu mpenzi wake wa zamani Boss Martha ambaye kwa miaka mitano waliishia kutemana wakirudiana.

Na katika kipindi hicho walifanikiwa kujaliwa mtoto wa kiume. Sasa baada ya Boss Martha ambaye alikuwa ni mchekeshaji kufariki, Mbosso akawa muwazi akafunguka mazito na kubainisha kwamba walizaa pamoja. Kwa kumsikiza Mbosso ungeona ni jinsi gani alivyokuwa anaumia kwa kuondokewa na mzazi mwenziwe huku akimwacha nyuma na kinda la miaka minne.

Kilichonipasua nafsi ni kuisikia familia ya Martha ikikana laivu tena peupe kwamba haimfahamu Mbosso na wala Martha hakuwahi kuwa na mahusiano naye na hawakupata mtoto. Na kama haitoshi hii ni familia ya mchungaji iliyotoa kauli hizi. Mchungaji,

mtumishi wa Mungu pamoja na familia yake akaamua kuuficha ukweli wa wazi. Ukweli ulio wazi kama meno ya ngiri.

Kilichofuatia ni kuharakisha yale mazishi ili kuua stori.

Mbosso alipojaribu kuhudhuria mazishi ya mzazi mwenziwe, wakamzuia. Wanaofanya haya kumbuka ni familia ya mchungaji. Sababu zao za kufanya yote haya ni kuwa Martha alitokea kwenye familia ya Kikristo na mwenzake akiwa ni Mwislamu.

Taarifa za ujauzito wa Martha tena kutoka kwa Mwislamu ziliwavuruga sana.

Familia hii ndio iliwaweka presha na kusababisha mapenzi yao kuvunjika. Ila baada ya kifo, ilikuwa ni wazi jinsi gani Mbosso alikuwa bado akimpenda Martha. Nina uhakika kapumzika huku akiilaani familia yake kwa kumfedhehesha baba ya mwanawe.

Familia ya Martha haikutetereka kabisa kwenye msimamo wao wa kupinga kuwa binti yao hakuzaa. Walikana kuwa ana mtoto.

Yule mtoto alikuwa akilelewa na dadake Martha kule Tabora huku naye akiwa Dar akiendelea kusaka maisha.

Dada mtu alipoulizwa, naye alikana akisema mtoto yule sio wa Mbosso na kwamba alimwokota barabarani kaachwa, hivyo akajipa jukumu la kumlea. Unafiki!

Uchungu

Kama ulimsikiza Mbosso, ungeona uchungu aliokuwa nao.

Sio jambo la kawaida kwa mwanaume kujitokeza na kujilazimishia mtoto tena sio kwenye karne hii ambayo wanaume wengi fursa kama hii wangeikumbatia na mikono miwili. Vile ni vidume ‘deadbeat’.

Pamoja na kuwa na uwezo wa kuitisha DNA, Mbosso alichukulia poa akaona asifanye drama kwa ajili ya mwanawe.

Wazazi hao kumkana yeye alisema hana kinyongo nao sababu hawajawahi kumpenda toka mwanzoni.

Hivi sasa nashangaa walitegemea Martha adeti nani? Mkristo mwenzake, Myahudi au nani? Na kama ingetokea hivyo kisha wapate mtoto, ingeleta tofauti gani?

Naandika nikiwa na moyo mzito, nauhisi uchungu anaoupitia Mbosso, naumizwa na unafiki wa familia ya mchungaji babake Boss Martha.

Ni vipi wazee siku hizi wanakosa busara? Tena wazee wa kanisa? Hivi ule msemo kuwa kitanda hakizai haramu, hawajawahi kuusikia?