Makala

DOMO KAYA: Kumbe ni kutuchocha tu!

February 7th, 2020 3 min read

Na MWANAMIPASHO

MWANZO kabisa acha nianze kwa kutoa risala zangu kwa mwendazake Rais mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi aliyefariki Jumanne wiki hii baada ya kuugua kwa muda.

Sikushangaa kuona jinsi taifa lilivyoguswa na kifo cha mzee Moi. Hakuna ambaye hakuwa na taarifa zake. Alipendwa, kuchukiwa na kuogopwa pia.

Kumbukumbu zangu kwake ni yale maziwa ya Nyayo. Japo sikufanikiwa kuyanywa sana kama wenzangu wengi walionitangulia, kwa miaka mitatu niliyopata, nilishukuru.

Sasa mzee kapumzika na atazikwa rasmi Jumatano ijayo. Mwachieni aende jamani, apumzike. Miaka 95 wengine wetu hata hatuna uhakika wa kuinusia.

Sasa basi, nikigeuza gia na kuzamia mambo yetu ya kupiga domo kama ilivyo ada hapa, leo mawazo yamenituma kwa Tanasha Donna. Bonge la msupa, kadamshi kweli kweli, ukimtizama lazima utadata tu.

Ndiyo sababu Diamond alidata naye baada ya kuachana na Hamisa Mobetto na kuamua kupita naye. Haikuchukua muda na ndani ya mwaka mmoja tu wa mahusiano, Mondi akamzalisha.

Lakini bwana sipo hapa leo kujadili maisha yao ya mapenzi, kwani hayanihusu. Mmh! Sio kwa sasa.

Linalonikuna mimi ni ule uzinduzi wa EP yake Donnatella alioufanya wikendi iliyopita jijini Nairobi.

Tanasha aliwaalika mastaa kibao ambao hakika hawakumwangusha, walifika kwa fujo kwenye ukumbi wa Sarit Center Expo kumpa sapoti.

Kilichonishangaza hata zaidi kama tu ilivyokuwa kwa wambea wengi tu, ni kile kitendo cha mpenzi wake Diamond, kuhepa uzinduzi wa sio tu mpenzi wake, lakini mama wa mwanawe wa nne.

Siku moja kabla ya uzinduzi, Mondi alitua nchini na kumsindikiza bae wake kwenye kikao alichokifanya na waandishi wa habari ila Siku yenyewe ilipofika, Jumamosi iliyopita, alikwea pipa na kurudi nyumbani kwao Dar es Salaaam. Kisingizio alichokitoa ni kwamba alikuwa na jambo la dharura la kifamilia alilohitaji kwenda kulishughulikia. Wengi hawakumwamini na mimi binafsi sikumwamini. Mwishowe nilikuja kumwelea huyu mswahili kwa nini alimtoka demu wake kivile badala ya kuwa mstari wa mbele kumsapoti kwenye uzinduzi wa EP yake ya kwanza.

EP hii Tanasha alikuwa ameratibia kuiachia Disemba mwaka jana lakini baadaye akaamua kusogeza tarehe mbele hadi mwezi huu.

Kipindi kile akiahirisha Novemba 2019 mtoto wa watu alisema kwamba, alishauriwa ni vyema kuiachia 2020 ili iweze kuwa kwenye nafasi ya kushindania tuzo mbalimbali za mwaka 2020. Lakini bwana kwa uzinduzi kama ule, EP hii ikiwa itaishia kushinda tuzo basi itakuwa ni kwa kupendelewa tu.

Toka Novemba hiyo, Tanasha aliishia kukesha mtandaoni akiipigia debe EP hii na kuwafanya wengi kutarajia uzinduzi wa aina yake kama ule uliofanywa na Diamond alipoachia albamu ya A Boy From Tandale hapa nchini, na kuacha ikizua stori kwa siku kadhaa.

Binafsi nilitegemea kuona Tanasha akiwa na utaratibu na mpangilio kama ule alioufanya Mondi.

Kwa namna Tanasha alivyoichocha EP yake, nilijua itakuwa bonge la shughuli sababu mwalimu mzuri wa hizi kazi, ndiye anayemkaza kila usiku. Imepita wiki toka imetoka EP hiyo lakini hakuna aliye na habari nayo.

Wajua ni kwa nini? Kwenye uzinduzi, Tanasha alikuja kuuza sura. Alikuwa kapendeza kweli, alidamshi kinoma lakini aliposhika mic kutema kazi zake, ikawa ni majanga. Huwezi kuamini sauti yake ilikuwa na mkwaruzo sikuamini, wakati mwingine aliimba nje ya ‘notes’ zile za nyimbo wakati hizi ni kazi zake. Wazo la kuwa na madansa hakuliwazia. Alikuwa na bendi lakini nayo ilionekana kuwa ovyo. Mwenyewe nikabaki kushangaa, hivi huyu binti kwa miezi yote hii amekuwa akifanya nini.

Baadaye shabiki mmoja alimchamba kwa uzinduzi huo ovyo. Tanasha akawa mwepesi wa kujitetea kwamba alikuwa tu na siku mbili za kufanya mazoezi. Hivi jamani toka Novemba alipoanza kuchocha kuhusu uzinduzi wa EP hiyo alikuwa akifanya nini? Au atasingizia alibanwa na majukumu ya kumlea mwanawe. Hata asithubutu, tumewaona wanawake wengi wakijifungua na kuendelea na mishemishe.

Kipindi akiwa anachocha mitandaoni, alikuwa akifanya nini badala ya kujihusisha na mazoezi? Hivi hakuwazia hata kufuata mawaidha kutoka kwa Mondi wake. Khuh! Huyu binti bwana huu muziki kweli kama vile analazimisha. Hakika Diamond alijua yaliyokuwa yakiendelea nyuma ya pazia na ndiyo sababu aliamua kumchorea giza kwenye uzinduzi ili aepuke aibu.