Makala

DOMO KAYA: Kwa sasa nitagomea hiyo stori ya Tanasha

March 6th, 2020 2 min read

Na MWANAMIPASHO

AISEE! Juzi Jumatano nimecheka sana.

Ni kama vile nilitarajia lakini ndugu wenzangu waandishi wa habari hawakukiona hicho.

Kuna mwenzangu mmoja hivi nilimwambia kweupe, kikao cha wanahabari kilichoitishwa na Mondi hiyo Jumatano asubuhi wala hakitamhusu hata chembe Tanasha Donna ambaye tetesi zinadai kuwa kaachwa.

Juma lote hili Tanasha katrendi kwelikweli baada ya ghafla kugeuka na kuwa ‘Motivational Speaker’.

Wajuaji kama mlivyo mkajijazia kuwa kaachwa. Sista alikoleza ubuyu kwa kuacha kumfollow, Diamond, dadake Esma, mamake Bi Sandra na hata kubadilisha jina la mwanao kwenye akaunti yake ya Instagram kwa kulifuta jina la babake.

Huku akiwa anatrendi Tanzania na Kenya, Mondi akawa wamepata fursa nzuri ya kufanya kitu kikubwa. Akiwa anajua macho yote yapo kwake, mzee baba akaitisha kikao na ndugu waandishi wa habari ili kutoa stori yake.

Ndugu zangu waandishi wa habari wa kule bongo naarifiwa walifika kwa fujo katika hoteli ya Serena kulikofanyika kikao kile.

Walikusanyana wote pale Serena Dar es Salaam ungedhani ni mkutano wa makundi ya kwaya tayari kushindana.

Kila ndugu yangu mwandishi wa habari akajipanga, wa kuandika akawa ana kalamu na karatasi, wenye kamera wakaziseti vizuri tayari kukamata video na picha za uhakika.

Wengine wakaamua kurekodi kwa simu, wengine walikwenda kabisa na makompyuta yao ili kuhakikisha kwamba wao ndio wanakuwa wa kwanza kupandisha exclusive kutoka moja kwa moja mlimani.

Diamond alishatusoma akatumaliza. Anajua kabisa yeye hutengenezea habari za kuvutia usomaji. Ilipofika muda wake wa kuongea jamaa akatangaza dili jipya aliloangukia kuwa balozi wa kampuni moja ya rangi kule Bongo.

Haya baada ya kusifia rangi waandishi wa habari walipata fursa ya kumuuliza maswali, wote wakaamua kumuuliza swali moja lililowapeleka kule: Ishu yake na Tanasha.

Hakuna aliyekwenda kusikiza stori za ubalozi wa rangi. Mondi alicheka akatabasamu sababu alitarajia swali hilo, lakini tayari alikuja amejipanga. Alilala akiwaza mbinu ya kulikwepa swali hilo. Na ndicho alichokifanya kwa kusalia kimya na kupuuza swali hilo.

Ndugu zangu waandishi wa habari mwisho wa siku waliondoka bure.

Nilikuwa nimeshahisi toka zamani kwamba hiki kitatokea. Diamond kwa miaka aliyodumu kwenye gemu hii, ameweza kujigeuza mfanyabiashara makini. Anajua kwenda na trendi. Anajua kuwachezea watu akili ili kuhakikisha kwamba daima anabakia kuwa stori.

Kwa kweli sitashangaa endapo visanga vyote hivi vitaishia kuwa ni kiki tu. Kesho nikimwona na Tanasha wala sitashtuka.

Ndiyo sababu mpaka sasa nimegoma kabisa kuandika stori kuhusu kuachana kwao mpaka pale nitakapoweza kukusanya taarifa za kutosha.

Wenzangu wanaotegemea stori wanazoposti wawili hawa, wataendelea kungoja. Utakuta pengine muda huu wapo pamoja wakitucheka kwa namna walivyotubeba ufala. Duh! Kweli huu mchezo hautaki hasira.