Habari Mseto

DOMO KAYA: Lion King: Tukubali tu yaishe

July 19th, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

FILAMU mpya ya Lion King itazinduliwa rasmi hapa nchini leo Ijumaa.

Kumekuwepo na mjadala mkubwa kuhusu uamuzi wa maprodusa wa kazi hizo kutumia majina ya Kiswahili pasi na kuwahusisha Wakenya kutokana na sababu kwamba mawazo ya utengenezaji upya wa filamu hiyo yalizalishiwa hapa nyumbani.

Nimewaona wasanii kibao kama vile Bien Aime wakilalamika jinsi wasanii wa Kenya walivyolalia maskio wakati raslimali zao zatumika kuwafaidi wengine.

Ndio ni kweli filamu ya Lion King (2019) kama tu ilivyotoka mara ya kwanza 1994 ikiwa ni miaka 25 iliyopita, imekopa sana rasilmali zetu.

Majina na maneno kama vile ‘Simba’, ‘Rafiki’, ‘Hakuna Matata’ na ‘Uishi kwa muda mrefu’ kwenye Soundtrack ya filamu hiyo Spirit, ni ya Kiswahili.

Mawazo ya uandalizi wa filamu hii yalianza 1988 na maprodusa wa Disney Jeffrey Katzenberg, Roy E. Disney, Peter Schneider na Thomas Disch kushikanisha vichwa na kuja na picha ya filamu hiyo.

Lakini ili kupata taswira kamili ya kile walichokuwa wakikusudia kukiandaa, walisafiri hadi Kenya na kutua katika mbuga ya kitaifa ya wanyamapori ya Hell’s Gate mjini Naivasha ili kufanya utafiti wa kweli. Baada ya hapo filamu ilikuja kutoka 1994.

Na sasa katika marudio wamekuja na wahusika wapya isipokuwa mmoja tu aliyetia sauti ya Mufasa. Miongoni mwa wahusika wapya ni Beyonce ambaye sauti yake kwenye filamu ya 2019 kavalia uhusika wa Nala.

Kelele ninazosikia kuwa tumelalia masikio naweza kuzifananisha na kilio cha samaki kwenda na maji. Hakika japo filamu hiyo inamilikiwa na kampuni hiyo ya Kimarekani, imekopa sana majina ya huku.

Wapo wanaolia kwa kuhusishwa kwa Beyonce badala ya wasanii wanaozungumza Kiswahili. Hii ni kutokana na Beyonce kulazimika kuzungumza Kiswahili kidogo. Wanachosahau ni hiki, kwamba mtu wanayemzungumzia sio msanii wa levo kama zao.

Huyu ni Beyonce, msanii mwenye jina lake, mafanikio yake, nafasi yake na hata zaidi himaya yake. Na hata ukiamua kumpuuza, wazo la kuwa ndiye mke wa rapa wa kwanza bilionea kuwahi kutokea, itatosha kukukalisha kitako.

Kina Bien na Vanessa Mdee wanalia kutohusishwa kwa msanii kutoka Ukanda huu. Ila swali lililopo ni hili, je, hao wana uwezo wa kuvutia mauzo na matangazo kama uhusika wa Beyonce?

Labda kuwakumbusha tu ni kuwa maandalizi ya filamu ni mawazo ya kibiashara na ndio sababu wakamwendea Beyonce ambaye sio mwigizaji. Kingine hata zaidi ni kuwa hatuwezi kulalamikia kutumiwa kwa maneno ya Kiswahili wakati hata hapa nchini zipo filamu nyingi zimeigizwa kwa kimombo ambayo ni lugha ya wenyewe.

Kingine mawazo yote na uandalizi wa filamu hii yalitokana na maprodusa wa Disney. Hamuwezi kupigia kelele kisicho chenu kwa sababu kimeonekana kukopa kwenu. Miaka yote hiyo tumeishi kuwa katika mazingira kama haya ila hatukuwahi wazia kuja na wazo la kutengeneza filamu hiyo. Sasa mgeni mjanja kaona ni nafasi nzuri ya kupita nayo, kafanikisha mradi tunabaki kulalamika.

Tujifunzeni kuwa wakweli.

Hili tulichukulie kama funzo na wala sio uwanja wa lawama. Nimewaona Magical Kenya kwenye mabango ya biashara. Tutajuaje kama nao hawakulipwa kuhusishwa pale. Tukubali yaishe, pale hatuna chetu. Wajanja walitumia maarifa yao kutugezia. Tulikosa nguvu, tukakosa uwezo wa kufanya walichokifanya sasa tunalalamika tunavyoibiwa. Kweli tuna kazi!