Makala

DOMO KAYA: Mapenzi yana wenyewe!

January 31st, 2020 2 min read

Na MWANAMIPASHO

OYA hivi mmesikia mapya?

Mzee baba Juma Jux katemana na Mchina wake Naika ikiwa ni miezi minne mitano hivi baada ya kukinukisha kweli kweli mtandaoni.

Hatukupumua, kwa picha zile aisee. Dah! Hata mimi mwenyewe nilipatwa na homa. Lakini ndio tena basi. Haya mapenzi bwana, kweli hayana maana kama tu alivyoimba Diamond.

Najua alipo EX wake Vanessa Mdee atakuwa kacheka kinoma pengine hadi ajikute katumbukia mtaroni. Utakuwa unajua ni kwa nini sio? Au lazima nikukumbushe? Basi kwa faida yako ni kuwa baada ya kutoka na Vanessa kwa miaka sita, waliamua kutemana. Hakuna aliyetegemea, hata shetani mwenyewe alishtuka. Malaika wa mbinguni vile vile walibaki na butwaa. Mashabiki wao wakashikwa na homa.

Sasa basi baada yao kuachana, Jux akawa wa kwanza kumtonesha kidonda mwenzake kwa kuanza kuposti picha za Naika. Naika baba kapiga plastiki sajari za kutosha mwili wake mtamu kama nini. Binti wa Kichina sijui wa Kiasia ana sura hadi anaumiza macho kumtizama. Kisha akikupigia yale mabikini ya kwake, Yarabi mama, yanakuwa ni mateso bila chuki.

Nakuambia hadi Vanessa aliumia baada ya kuona Jux kasonga mbele tena kwa kuopoa kifaa. Aliumia hadi mwenyewe akakiri redioni kwamba kila alipomwona Jux akiposti Mchina wake, kitu kilikuwa kinabana kifuani. Ikabidi Vee Money naye arudishe mkono tena kwa uzito. Huyo akajitahidi na miezi michache akaanza kutupostia picha za oga maarufu anayeigiza kule Marekani Rotimi Akinacho. Aisee! Vee alilipiza kisasi na mpaka sasa hatupumui kwenye mitandao ya kijamii. Picha anazozimwaga kule akiwa na Rotimi, zinatosha kumpa aliye singo, presha ya damu.

Lakini nilimwelewa Vanessa. Lazima angelipiza kisasi kivile na ndio sababu ninasisitiza kuwa sasa hivi kama kunaye aliye na furaha baada ya Jux kutoswa, basi itakuwa ni yeye.

Ya kwake yanamwendea vizuri na bora awe anaomba dua mapenzi yao yafike mbali. Ashasema kuwa anamwona Rotimi kuwa mwanamume atakayemwoa. Mmh! Sina uhakika. Wanaume tulivyoumbwa sisi, tena kwa umaarufu ule manze. Acha tu.

Lakini pamoja yote tisa, kumi mawazo yangu yapo kwa Jux. Namwona jamaa anajikausha tu. Baada ya kuachwa kaamua kwenda zake Zenji yaani Zanzibar ambapo anakula bata sana. Na sijui kama ni sadfa au vipi sababu pia naye Huddah yupo huko huko Zenji naye akila bata. Kwa picha wanazotupia ni kama vile watakuwa wamekutana au wapo pamoja. Bora tu asijisahau akazama kwenye penzi lake.

Lakini pia nafikiri haya matukio yatakuwa funzo kwake. Unaweza ukawa kwenye mahusiano kimya kimya bila taarifa kwa umma. Sasa ona tupo hapa tunamchambua. Khuh! Jux kanikumbushia mashairi ya Diamond; “Haya mapenzi bwana hayana maana, yalinifanya mi nichekwe, sababu yake nishagombana, nikatukanwa lakini akanipiga teke…”