Makala

DOMO KAYA: Masista, inauma lakini itabidi mzoee

November 8th, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

KUNA wimbo Ethic wameachia juzi Tarimbo ambao umewakuna pabaya kina dada.

Kikweli huu wimbo huwezi kuusikiza sebuleni na dada zako, mamako au mtoto yeyote yule wa kike. Ni wimbo wenye mashairi machafu.

Maudhui ni ya udhalilishaji wa mtoto wa kike. Hauna stara wale tija au chembechembe yoyote ile ya maadili.

Saa masista wamepiga kelele kweli, wapo wadau wasanii wa kike wamejitokeza kukashifu kazi hii.

Kinaya ni kuwa, wakati wakiendelea kukashifu ndio nao wimbo wenyewe unazidi kupata umaarufu.

Pale YouTube kwa mfano, Jumatatu ilikuwa imefikisha Views 300k na hesabu juu. Jana Alhamisi tayari ilikuiwa ishafikisha views laki nane ikiwa inakimbilia milioni.

Na kama haitoshi kwenye Youtube Kenya ndio video ambayo ilikamata nafasi ya kwanza kwa video zilizotrendi Youtube tangu kuanza kwa wiki.

Hii inawaambia nini? Majibu tayari mnayo. Kingine mnadhani mnaweza kunisadikisha kwamba hao maelfu ya walioutizama ni makaka bratha tu? Tutakuwa tunadanganya.

Sitaki nieleweke vibaya, sio kwamba nawatetea Ethic ila najitahidi kuwaza katika uhalisia wa matukio. Wale wamnaopiga kelele kuhusu ubovu wa wimbo huu wala sikuwasikia mkipayuka kundi hili lilipoachia hiti yao iliyowatambulisha kwenye gemu Lamba Lolo.

Kazi ile pia ni chafu tena ya udhalilishaji. Lakini hamkuona hilo. Au tuseme sheng ndio hamkuelewa. Au pengine mwapenda kulamba lolo hivyo mkaona isiwe tabu. Mlikuwa bize wenyewe mkiusifia. Nyie ndio mliwapa madogo hawa nguvu kuendelea kuachia tungo za dezaini hii. Sababu mpaka leo bado sijauona wimbo waliouimba usiowadunisha nyie kina dada zetu.

Sasa leo kwenye Tarimbo wamepiga vesi moja pale “…bas, bas joo kama ana maringo, mi hupenda chapa na tarimbo, mi huchapachapa nakayaga namwaga bila permission” na ghafla mumeshtuka na kukurupuka kama mtu aliyechomwa na mwiba makalioni.

Hivi kwa nini tunakuwa ‘Waswahili’ sana? Hakika mmepiga kelele mpaka yule bosi wa KFCB Ezekiel Mutua kagutuka. Kajaribu kutishia madogo wakamatwe ila nafikiri DCI wana kazi kubwa za kufanya.

Kawandikia Google akitaka wauondoe wimbo huo lakini tena bwana huwezi kumpangia mtu anavyopaswa kufanya biashara zake.

Ukweli wa mambo ni kuwa tunaishi katika karne ambayo kuna mumomonyoko wa maadili kutokana na athari za mataifa ya Magharabi. Sasa kama wao kina Nicki Minaj hutunga mashairi machafu na kisha kuzipamba video zao na mademu nusu uchi unategemea Ethics wafanye nini wakati watu kama wale ndio role model wao.

Lakini pia tukiachana na Ethics, zipo kazi nyingi tu ambazo zimeachiwa siku za hivi karibuni ambazo zote ni za kumdunisha sista. Sailors wanapouliza hao mademu wasimame au wainame, wenyewe nimesikia mkiitikia ‘wainame’.

Sasa kelele za nini tena? Hao hao Sailors wakiangusha kibwagizo ‘Wamlambez’ nyie nyie mnajibu ‘Wamnyonyez’. Leo sasa mumegeuka wanaharakati wa maadili. Hehehe! Aisee msinichekeshe.

Nikiachana nao pia kuna huyu dogo wa ‘Zimenishika’, Zzero Sufuri anao wimbo Matiati hivi mnataka kujifanya mashairi ya kazi hiyo nyie wanaharakati wa maadili hamjayaskiza. Hata mjomba wenu mtetezi Mutua nashangaa kapitwaje.

Basi kuna mshoshoro mchafu kwenye wimbo huo ambao Zzero anasema “…mambo Lucy napenda hako kapusi, kakuwe kabrown sanasana tu keusi, kako na tunywele tusoft ka tausi. Ni karefu sana mimi hukapimaga na uzi na venye kuna joto si ukatoe ndani ya kamisi najua kanasikia njaa toka juzi..”

Mbona sijasikia kelele za kukashifu uchafu huu? Inauma lakini itabidi tuzoee.