DOMO KAYA: Napenda kiki ya dizaini hii

DOMO KAYA: Napenda kiki ya dizaini hii

Na MWANAMIPASHO

NAONA watu wanamwingilia sana Eric Omondi baada ya jamaa kuanika mjengo wa kifahari anaodai kuumiliki maeneo ya Karen.

Kadai kaununua kwa kima cha Sh141 milioni.

Baada ya kuposti mjengo, wapekuzi wa kamati ya roho chafu waliibuka na risiti na kumtumia bloga Edgar Obare kuthibitisha kuwa mjengo sio wake.

Kulingana na zile risiti, mjengo huo ni ‘Airbnb’.

Baada ya jamaa kuanikwa, alijitokeza na kuonyesha hatimiliki ya ploti hiyo.

Akijitetea, Eric alidai kafanya kazi kwa miaka 14 hivyo kumiliki mjengo kama huo sio ishu kwake kwa sababu sanaa anayoifanya yeye inamlipa vizuri. Lakini bado tu kamati ya roho chafu iliibuka tena na risiti mpya na kudai zile hati alizoonyesha zilikuwa feki.

Inawezekana ikawa ni ukweli jamaa anamiliki nyumba, au ikawa ni kiki tu. Watu wamechamba sana ila mimi nilipo sishangai.

Ndivyo walivyo hawa wasanii. Kazi kwao ni kuibuka na kiki ili waweze kutrendi. Na katika kutrendi huko ndivyo wanavyojitengenezea riziki. Natamani sana kuamini kuwa ule mjengo ni wake ila na mimi pia nina dukuduku zangu. Lakini kama nilivyosema, siwezi kumlaumu. Napenda kiki ya dizaini hii. Ni kiki ambazo kwa mtazamo wangu zina mwelekeo.

Kusema kweli Eric hujituma sana na ni haki yeye kuwa na mali ya kiwango kama kile hata ikiwa bado hajafikia upeo ule. Ila pia najua sio wengi wanaopenda kuwaona wenzao wakifanikiwa. Ndivyo binadamu tulivyo.

Wengi wetu tumekodisha wivu chumba kwenye mioyo yetu. Sisemi tusikemee maovu, ila pia tusiwe na mioyo ya kuona wenzetu hawastahili kupata vizuri na vikubwa.

Lakini hiyo sio mada ninayoilenga mimi. Kwa wanaomchamba Eric kwa jinsi anavyojisifia na kuringisha mali yake, msisahau sio staa wa kwanza kuibuka na kiki kaa hizi. Hata kule majuu wasanii wengi wanafahamika kwa kuibua kiki kwa lengo la kujitafutia riziki.

Kwa mfano hivi majuzi mwigizaji wa Fast & Furious Tyrese Gibson, kaomba msamaha baada ya kuwabeba mashabiki wake kimalenge. Jamaa alizua kiki kuwa kaachana na demu wake Zeile Timothy wakati kumbe ni uwongo.

Lengo lilikuwa ni kuzua kiki ili amwezeshe demu wake kupata wafuasi wengi kwenye Youtube kwa kutizama video aliyoposti baada yao kudai wametengana. Hii ni hali ya utafutaji tu.

Kumbuka Tyrese kwa fedha za Kikenya tayari jamaa ni bilionea. Ila bado anazua kiki za kipuzi ili kumsaidia mpenzi wake kusaka fedha zaidi. Ndio maana sioni kwa nini na Erico tuwe na machungu na kiki zake. Anahangaika tu kusaka riziki. Au anatamani tu kuwa na mjengo kama ule.

Wajua hata Lil Bow Wow kawahi kudaiwa kuwalipa ‘mashabiki’ pesa wamkimbize barabarani ili kuchora taswira jinsi alivyo maarufu. Ndiko kutafuta huku.

Napenda kiki za kiubunifu kama hizi.

Kiki nisizopenda ni kama hizo za kina B Classic eti ooh kaacha muziki kawa mekanika, halafu kesho anaachia ngoma.

Au zile alizokuwa akifanya Otile, anaondoa ngoma YouTube kisha anairejesha baada ya kupiga kelele ili iweze kupata views.

Hizo ni kiki za kishamba. Kibaya hata zaidi, wasanii wamekuwa wakiigana kwa kiki za dizaini hii.

You can share this post!

Kafyu itaondolewa karibuni, asema Balala

Jinsi ya kuandaa mkate wa maziwa