Makala

DOMO KAYA: Pwagu kapatana na pwaguzi

June 7th, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

HAYA buana sijui nianzie wapi.

Nimemsikia bwana mkunaji akilalamika eti kaibiwa wazo alilokuwa nalo la wimbo mpya aliokuwa akiuandaa.

Wimbo huo kauita Chuchuma.

Sasa Bwana Mkunaji kwa wasiomfahamu, Willy Pozee hivi majuzi kashoboka kwenye Instagramu yake kuwa kuna msanii mwenzake kutoka taifa jirani anajaribu kumkwepua wimbo huo.

Anadai kuwa kwa muda Wakenya wamekuwa wakiwapa sapoti sana wanamuziki wa kwao, hivyo kumwona akijaribu kumwibia wazo la wimbo huo ni jambo ka kushangaza na kuumiza nafsi.

Dogo huyu mpenda madrama kadai eti huyo msanii ambaye hakumtaja jina, kafanya kuiba wazo lake la wimbo huo baada ya mazungumzo yao ya uwezekano wa kufanya kolabo kuvunjika.

Baada ya kupikicha kwa haraka, wengi nikiwemo tulibaini kuwa alikuwa akimzungumzia Rayvanny ambaye hivi majuzi aliposti video fupi akiandaa wimbo aliouita pia Chuchuma.

Sasa kwa kauli ya Pozee ni kuwa jamaa anajaribu kumfunika. Na ametishia kulipiza kisasi kwa njia anayoifahamu mwenyewe.

Kumbuka huyu Pozee tayari anayo kolabo na Rayvanny Mmmh ambayo imefanya vizuri sana ikiwa na zaidi ya ‘views’ 6. 3 milioni kwenye YouTube. Wimbo ni wake Pozee.

Nashindwa kuelewa kwa nini kama waliweza kuelewana na kufanikisha mradi huu, ni vipi walishindwa kuelewana kwenye Chuchuma hadi ikamlazimu mwenzake kuchuchumaa na kupita nao.

Lakini hilo hata halinihusu kabisa.

Linalonikuna kichwa ni malalamishi ya Pozee.

Ukiniuliza mimi, kwa wasanii ambao ni wanafiki na wasio wakweli licha ya kujaliwa kipaji, basi huyu Pozee anaongoza.

Wakati akilalamika kuibiwa, kaibuka msanii mwingine kutoka kaunti 001, Kelechi Africana anayesema wazo halisi la wimbo ni lake.

Alirekodi kionjo na kuposti kwenye akaunti zake za kijamii na bwana mkunaji alipata kukiona.

Akapenda wazo na kuamua kumsaka Rayvanny kwa ajili ya kolabo ila kwa wizi huo, ‘karma’ kampata, malipo ni hapa hapa duniani.

Nimefanya kumwamini Kelechi sababu kumwamini Pozee ni taabu tu.

Inaweza ikawa naye Kelechi ana mambo yake au anasaka kiki, ila kama ni suala la yupi wa kumwamini, heri niwaamini Kelechi au Rayvanny.

Unaweza kusema nina chuki au kinyongo na Pozee. Shauri yako bwana. Hainipunguzii kitu. Ila kwa kwendana na taarifa na kumbukumbu, tunafahamu fika Pozee ni mtu wa aina gani.

Huyu ni msanii ambaye kipaji chake ndicho kimemweka kwenye gemu ila kimaadili na kitabia ndio kaoza kaozeana.

Muulize hata Jalang’o atakwambia sababu pekee ya Pozee kutochukuliwa kwenye Coke Studio toka ilipoanza ni tabia zake hizo chwara.

Lakini nikirudi kwenye mada, huyu Pozee anayedai kuibiwa wimbo leo, aliwahi kushtumiwa na msanii Bahati 2015 kwa kumwibia wimbo Mapenzi. Ni kitu kilichowaingiza kwenye bifu mbaya iliyodumu kwa zaidi ya mwaka.

Pia mwaka 2018, wimbo Bora Uhai aliomshirikisha rapa Khaligraph Jones alidaiwa kuwaibia wasanii chipukizi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta baada ya kumtumia kuusikiliza. Hili sina ukweli nalo kama lile la Bahati sababu ithibati ilionekana.

Nakumbuka wakati wa bifu yake na Bahati, kuna mmoja wa mashabiki aliyesema kuwa Pozee kwa wizi wa nyimbo tu, anao uwezo hata kuiba ‘Songs of Solomon’ kwenye Biblia. Mie namchekea bwana mkunaji tu. Kama Rayvanny kamwibia, basi naona jomba alijiona pwagu lakini sasa kakutana na pwaguzi. Acha mchezo uendelee. Mechi ni dakika 90. Eish!