Makala

DOMO KAYA: Tuko rada yenu tena sana!

September 13th, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

HABARI za kwako ndugu yangu? Za tangu wiki iliyopita? Natumai Allah kakujalia neema zake kiasi cha wewe leo hii kutua tena kwenye ukurasa wako huu uupendao.

Hivi umepata kuiona video inayozunguka mtandaoni ikimwonyesha rapa Kristoff na rapa wa kike Kush Tracey kwenye tukio kama la kifumanizi hivi?

Kwenye matukio ya video hiyo inayosemekena kutokea Jumapili iliyopita, Kush na Kristoff wanaonekana wakiondoka klabuni huku wameshikana mikono.

Wapo kwenye mwendo wa asteaste huku Kush akionekana kutatizika kidogo na viatu vyake vya inchi sita au tano, mimi sijui. Yaani kwa mwendo ule hakika ilichora taswira ya watu wawili wanaokwenda kudandiana.

Sasa wanapokaribia lilipoegeshwa gari la Kristoff, ghafla anatokea Yvonne Darcq kutoka kusikojulikana na kuanza kumshobokea rapa huyo akimshtumu kwa kumchepukia.

Tena anamfuata na maneno makali akimshtumu kwa kuwa na tabia hiyo kwa miaka mingi waliyodumu kama wapenzi. Hapo ndipo kidogo napozi na kunywa maji kisha naibua kumbukumbu, “Hivi sio hawa tu walioishi kukana kuwa kwenye mahusiano?”

Kwa kila mahojiano waliyoandamana kufanya kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano iliyopita, Kristoff na Yvonne wameishi kukana kuwa wanadandiana.

Ila sasa kwenye fumanizi, Yvonne alicharuka na kumshutumu kwa kuwa na tabia za kumchepukia. Khuh! Showbiz hii mbona itanitoa uchizi.

Nikikurejesha tena kwenye ile video, utamwona Kush akiwa anacheka wakati Yvonne akiendelea kushoboka. Kisha anamfuata Kush na kumweleza hana tatizo naye badala yake anamgeuzia hasira Kristoff. Mtoto wa kiume naye anajitetea kuwa alikuwa anamfikisha tu Kush nyumbani kwake kisha yeye akwende zake nyumbani.

Video ile imeniacha na maswali kibao. Ina kama ukweli na uwongo hivi. Hivi itakuwa ni kiki, sababu ukiitathmini kwa makini ni kama vile imeigizwa? Hivi ni kwa nini Kush awe anacheka wakati wamefumaniwa? Ni kwa nini Yvonne hammiminii hasira Kush wakati wanasema mshikwa na ngozi naye pia ni mwizi?

Hivi Yvonne alitokea wapi ghafla na kuanza kushoboka?

Yule aliyekuwa anarekodi ilikuaje akajikuta kwenye eneo la tukio tena kwa wakati? Mbona hatumwoni Kristoff au Kush wakijaribu kumzuia asiwarekodi sababu ile ni fedheha. Lakini kwa nini Kristoff aamue kuunda kiki sasa na jinsi anavyopenda usiri? Tena Yvonne na Kristoff waunde kiki kwa kufichua madai ambayo wameishi kukana eti kuwa ni wapenzi? Ila kama matukio haya ni kweli, pole zangu zimfikie Yvonne.

Huku nikiwa na hayo maswali kichwani, Kush naye kweli kawa ovyo. Kule kuokoka kweli sasa hamna maana, au ndio anafuata nyayo za Willy Paul? Achunge asije akakanyaga kinyesi.

Au pengine labda atakuwa anamisi kuangaziwa kama ilivyokuwa alipokuwa na Timmy Tdat. Itakuwa Switch TV haimpi kiki ya kutosha jinsi alivyotegemea? Ule ndio wokovu, kusaka kiki, au hata kama sio, anaona freshi kujihusisha tena na utundu wake?

Hakika katu chui hawezi kubadilisha madoa yake. Huyu Kristoff alisema leo atadandia kama mathree, mwenzake akajibu mapigo kuwa hawezi kumdandia kama mathree, sasa naona wameamua kudandia kiki. Ovyo nyie! Tushawasoma! Haya basi achieni wimbo mpya tunasubiri. Ole wangu nisiwe nimekosea.