DOMO KAYA: Tuseme kajitakia mwenyewe

DOMO KAYA: Tuseme kajitakia mwenyewe

Na MWANAMIPASHO

NIMEMWONA Georgina Muteti, demu wake Khaligraph Jones akimtetea sista-du Tanasha Donna.

Georgina anadai kuwa wadau humwonyesha chuki sana Tanasha mitandaoni bila ya sababu na kwamba sio poa. Kweli sio poa. Najua Georgina na Tanasha ni mtu na shogake, toka alipofanya kazi na ninja wake Khaligraph lazima tu usista-du ungeingia.

Napenda alivyomtetea, mwenyewe hapa natamani kuwa na marafiki wa dizaini hiyo ila ndio basi sijabahatika. Lakini swali kubwa ninalojiuliza mimi, hivi ni kwa nini Tanasha pamoja na uzuri wote ule anachambwa sana? Naamini kila mtu ana sababu zake na hizi hapa ni fikra zangu.

Mwanzo kabisa sio tu Tanasha anayechambwa, maceleb wote naona wakichambwa kila kukicha. Mulamwah nusura aache komedi, kisa kuchambwa. Natalie Tewa kaacha kutengeneza video zake za Youtube, kisa kuchambwa; Zari The Boss Lady anachambwa kila leo, kina Huddah Monroe, Vera Sidika na wengine wengi tu. Wapo mastaa kibao wengine waliokiri kuwa nusura wachizi kwa sababu ya chambo za mitandaoni.

Niliwahi kusema hapa tangu zamani kwamba ustaa ni mzigo wa mwiba, lazima uwe tayari kuubeba. Sielewi ni kwa nini Georgina haelewi hili. Kuchambwa kitu cha kawaida na kinachangiwa na mambo kadhaa. Inawezekana ikawa ni wivu kwa sababu Tanasha ni staa lakini pia inawezakana ikawa imechochewa na tabia zake. Tanasha kabla hajawa maraufu alivyo, amekuwepo kwenye gemu akivuruga tu.

Kama tu Natalie Tewa, hawa ni warembo ambao wamepata umaarufu sio kwa kazi zao wanazozifanya ila zaidi kutokana na mahusiano yao. Haipo hata siku moja niliyosikia Natalie katrendi kwa sababu katengeneza Vlogg kali. Ila daima ametrendi kutokana na kashfa za mahusiano yake. Mara yake ya mwisho kutrendi ilidaiwa kwamba anatoka kimapenzi na Gavana 001.

Natalie alipata umaarufu huu baada ya kumchepukia aliyekuwa mpenzi wake Mganda Rnaze. Amekuwa na skendo kadhaa za kuwabadili wanaume. Mwenyewe kawajengea mashabiki wake taswira kwamba, upeo aliofikia umechangiwa zaidi na wanaume aliojihusisha nao. Ndio picha sawia na yake Tanasha, sema wahusika ndio tofauti.

Huyu Tanasha aliwahi kudaiwa kutoka kimapenzi na AliKiba ingawaje alishakana na kusema kuwa ukaribu wake na staa huyo ulitokea waliposhuti video ya wimbo wake Nagharamia0. Pia aliwahi kuwa kwenye mahusiano mafupi na mwigizaji mtanashati Nick Mutuma. Wakati huu Mutuma alikuwa kaachana na demu wake wa sasa Bridget Shighadi.

Zari alipomtema Diamond kwa kumchepukia, aliwahi kufunguka na kusema kwamba Tanasha aliishi kukesha kwenye ‘timeline’, ni kama vile alikuwa akimtamani mpenzi wake. Tafsiri ya hii ni kuwa, Tanasha labda alikuwa akipekuapekua Zari ni mwanamke wa aina gani na anafanya nini mpaka apendwe na Mondi. Kweli Zari alipomtema Mondi, miezi michache baadaye Tanasha akarithi nafasi.

Kwa mtu wa mienendo hii anayewajengea mashabiki wake picha kama hizo, Georgina atategemea vipi apendwe. Juzi baada ya kumpelekea mwanawe akamcheki babake, mlimwona kabisa akijisugulisha kwa Simba asiyependa kuona sketi ikipita mbele yake. Mliona wakishikana mikono na huyo EX wake. Alionyesha kabisa bado anamdai licha yake kumchamba sana walipoachana.

Zari alipowapeleka wana kumcheki baba yao, wala sikuona akifanya tabia kama za Tanasha. Sio ajabu Wakenya waliishia kumkeshea mitandaoni wakidai kuwa kwa namna alivyokuwa akijibebisha kwa EX wake, ataishia kwa kupachikwa mimba ya pili na kisha aachiwe mbali.

Nilipomwona akimsugulisha kwa Mondi, niliwaza sana nikikumbuka alivyomchamba kwa kumwachia majukumu ya kumlea mwanao pekee. Kwa sababu hizi, najua Georgina hawezi kunielewa. Ila mimi namwelewa, anamtetea kwa sababu yule ni shosti wake. Basi jamani, mbona asimshauri namna ya kulinda heshima yake hasa mitandaoni?

You can share this post!

KIKOLEZO: Maskendo kibao yachoma picha

EPL: Liverpool wajifufua ugenini wakipiga tena Tottenham...