Makala

DOMO KAYA: Wakomeshe kiherehere!

August 2nd, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

WIKI iliyopita makala ya Bambika yaliangazia jinsi lebo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki zinavyohangaika kufanya biashara na hasa hapa nyumbani.

Mpaka sasa hamna lebo iliyostahimili vishindo hapa nchini na kuthibitisha kwamba kweli hii ni biashara tamu.

Nisichokielewa ni kwamba licha ya ugumu wa kuisimamisha lebo na kuifanikisha, wasanii kila kukicha wanazidi kuonyesha tamaa yao kutaka kuwa wamiliki wa lebo. Ila utafiti wangu umenifanya kupata majibu. Tatizo kuu ni kiherehere. Eeh!

Wengi wa wasanii hawa wana kiherehere tu. Wanataka kuonekana kuwa wana uwezo wa kumiliki lebo wakati hamna kitu. Hawajafanya utafiti kuelewa ni nini maana ya kumiliki lebo.

Wanahisi kwamba kuwa msanii ni tiketi tosha ya kuanzisha lebo. Sijui nani aliwambia hilo. Wengine wanapopata visenti vidogo wanawashwa na kuona kama vile wamefika.

Kwenye makala hayo, ziliorodheshwa lebo kadhaa ambazo zilikuja na kupita. Candy & Candy iliyomilikiwa na Joe Kariuki, iliingia kwenye gemu kwa fujo ila baada ya miaka mitatu walifunga duka.

Pia ipo Kaka Empire ambayo ukiitathmini kwa kina utagundua kuwa ile ni lebo ya kiusimamizi tu wala hamna kikubwa pale. Sishangai kwa nini Avril, Timmy T Dat, Arrow Bwoy wote walitoka lakini bado wanasumbua chati.

Grand Pa tu ndiyo lebo unayoweza kuipa heshima zake. Kwa takriban mwongo ilijaribu, iliwatengeneza wasanii wengi na kuwafanya mastaa lakini kuta zake zilipopata nyufa kidogo tu kwa wasanii kadhaa kuondoka, nayo ikaporomoka. Baada ya ukimya wa miaka miwili toka ilipoporomoka, ilirejea tena mapema mwaka huu ikilenga kufanya kazi tu na wasanii chipukizi.

EMB Records ya Bahati nayo vile vile, baada ya miaka miwili, wasanii wakang’oka na kuiacha ikiporomoka huku mumiliki Bahati akilia kuingia hasara ya zaidi ya Sh6 milioni alizokuwa amewekeza.

Mwenyewe alikiri lebo haikuwa ikimpa faida. Sema jina tu. Aprili mwaka huu alijaribu tena kuifufua kwa kumsaini msanii Danny Gift ila taarifa tulizozipata ni kwamba jomba tayari keshaondoka EMB hata kabla ya miezi mitatu kumalizika.

Nakumbuka pia kipindi fulani mwanamuziki Habida baada ya kurejea kutoka Afrika Kusini alikokuwa amehamia kwa miaka mingi na mumewe, alidai kuwa alipania kuanzisha lebo yake ila ya wasanii wa kike tu.

Mmiliki wa Grand Pa, Reffigah alimcheka na kusema hilo haoni likiwezekana.

Habida akashika machungu ila baadaye alikuja kukiri kwamba hataweza.

Naye mzushi Willy Paul mara tu baada ya Bahati kuanzisha lebo yake naye kwa kiherehere chake akaanza mikakati yake na kuzalisha Salidido Records aliyosema tayari imewasaini wasanii wawili na hivi karibuni atawazindua.

Kauli hiyo aliitoa Aprili, imepita miezi minne sasa. Naona ni kama vile maana ya ‘hivi karibuni’ iliharibika.

Haya tumgeukie Otile Brown naye alianzisha lebo yake, Just in Love mwezi uliopita na kumsaini msanii Jovial baada ya nyimbo zao mbili kufanya vizuri. Hata mwezi haukuisha kabla Jovial kuondoka akisema tofauti za kimkataba ndio tatizo na kuwa ni Otile aliyeamua kuvunja.

Nimegundua kitu kimoja. Wasanii wote hawa ni kama vile wanajitahidi kushindana na Diamond Platnumz aliyefanikisha lebo yake ya Wasafi.

Ndio lebo bora zaidi katika Ukanda huu licha ya kusemekana inawabania wasanii sana.

Ilimchukua miaka kadhaa kabla ya kuja kuisimamisha na kipindi chote hicho alikuwa anafanya utafiti, wanachoshindwa kukifanya wasanii Wakenya.

Mwanzo alisaka wadau watatu wenye sifa za umeneja, akampata Sallam Mendez, Babu Tale na Saidi Fella ambao kwa miaka mingi wamejihusisha na sanaa.

Kisha akaamua kusaka msanii mmoja mwenye kipaji cha ukweli. Ndivyo alivyoanza na Harmonize na kuwekeza kwelikweli kwake kumboresha.

Kisha akamfuata na produsa, mpiga picha na mambo kama hayo.

Taratibu zote hizi hakuzifanya kwa pupa, ilichukua muda. Hata wakati anakuja kutambulisha Rayvanny kama msanii wa pili pale WCB, ilichukua miaka miwili.

Tatizo na kina Bahati wetu hawa, wakiamka leo, wanataka kumsaini kila mtu wanayemwona mzuri. Nyoo!