Makala

DOMO KAYA: Wambea tumeachwa hoi!

November 22nd, 2019 2 min read

Na MWANAMIPASHO

WAMBEA juzi tumeachwa hoi jamani.

Tumebaki kuonekana mafala. Kuna picha mbili zilizojitokeza ambazo zilituacha kuoneakana wapuzi sisi wanazengo wenye tabia ya kujaza susu pasipotuhusu.

Hivi ni wangapi kati yenu mliamini kabisa kwamba kakake nyota wa Hollywood Lupita Nyong’o, Peter Nyong’o kwamba alikuwa ni ‘kaka poa’? Kitaani naskia wakiitwa masala wanaoichezea Team B. Nani kati yenu aliamini. Hebu nyanyueni mkono.

Siwezi kumhukumu yeyote aliyeshikwa na fikra hizi sababu kwa staili ya mavazi ya Peter basi hamna kingine ambacho ungewazia zaidi ya hicho.

Mara ya kwanza mimi kumwona kisha nikapaniki kidogo ilikuwa ni kwenye hafla ya uzinduzi wa filamu ya Star Wars kule Marekani ambapo alimsindikiza dadake Lupita. Siku hiyo, Peter alikuwa amepiga pamba kali nyeusi lakini kichwani akafunga kanga kabisa. Leso nakuambia.

Kisha puani akawa ametoboa na kupitisha kipini hivi katikati ya mshipa wa ndani wa mapua yake.

Kule kubana pua wala hakukunishtua sana lakini ile kanga kichwani, ilianza kunifanya kwumona kivingine kabisa. Kabla sijakaa sawa miezi michache baadaye, Peter alihudhuria shoo ya Blankets Wine akiwa amepiga rinda moja safi aina ya Maxi.

Rinda lile njekundu lenye michirizi meupe ndio sasa lilinifanya kusadiki kwamba mimi na yeye tulikuwa tukizichezea timu mbili tofauti yeye akiwa B mimi nikiwa A.

Kidogo kidogo siku moja akaamua Peter kukoleza urojo kwa kutupia picha za shuti aliyofanya akiwa amevalia thong nyekundu. Yaani zile chupi za kina dada zenye kamba tu ambazo zivaliwapo, husitiri ule mto wa mbele tu na kisha kamba moja kupita katikati ya vile vilima vya nyuma huku vikiacha mambo mengine yote wazi.

Sijui kama umeipata picha hiyo vizuri? Sasa Peter na vikalio vyake vigumu kutokana na vilivyoonekana licha yake kuvipaka mafuta kweli kweli, aliamua kuvalia hiyo thong nyekundu, akafunga kitambaa chekundu kichwani na kisha kuvalia viatu vyenye visigino virefu.

Picha ile haikudumu sana kabla yake kufuta. Lakini wambea tulikuwa tayari tumeshaiwahi na wengi wetu tulijijazia mengi.

Sasa juzi kati Peter katuaibisha baada ya kujitokeza wazi wazi na kumchumbia mpenzi wake wa muda mrefu Wanja Wahoro.

Mwenzako nilibaki kujicheka. Kumbe kweli umthaniaye ndiye kumbe siye. Kumbe bratha kaka hayupo kule. Lakini ninachoshindwa kuelewa ni hiki. Peter alifanya yote yale kwa sababui gani. Kusaka kiki? Ya nini? Au ni tabia za watoto matajiri wanapokosa kazi? Sababu babake ni gavana.

Nakumbuka Peter akisema anapendezwa na mavazi ya kike sababu zinamfanya kujihisi huru kujieleza.

Lakini nami najikuta nikiwa na maswali kibao. Ikiwa kweli huko ndiko kujieleza, ni kwa nini basi kuna aina mbili ya mavazi, ya mademu na wanaume?

Tunaishi katika jamii ya Kiafrika ambapo masuala ya mapenzi na mahusiano huchukuliwa kwa uzito. Licha ya kuwa kuna wanaharakati wanaopambania mambo haya ya Kizungu, bado sehemu kubwa ya jamii kwa ujumla haikubaliani nalo.

Hii ndio sababu wengi huhisi ni kama vile wanabaguliwa. Lakini wanachosahahu Kenya ni mojawepo ya taifa ambalo sheria zake zinapinga mienendo ya aina hii ila tu hizi ni sheria ambazo hazifuatiliwi.

Sijui Rais Museveni angelimfanyia nini Peter endapo angekuwa Uganda sababu kule kina ndugu zetu wanaochezea Team B wala hawachwi salama. Ingelikuwa Uganda kisha mabaya yakamkuta Peter wakati kumbe mwenzenu anachezeaga Team A, sijui ingelikuwaje.

Ni mawazo tu.