Na MWANAMIPASHO
KENYA ni nchi speshio.
Wakati mwingine huwa nakaa nakuwaza kama mataifa mengine hushuhudia drama ambazo sisi Wakenya hupitia kila kukicha.
Wiki hizi mbili zilizopita zimekuwa nzito kwa kweli. Vituko kila upande. Kila ukigeuka unakutana na la kukuchekesha na kukushangaza wakati huo huo.
Hivi mwanzo mlimwona Eric Omondi alivyoruka kule juu kwenye ‘Maria’ polisi walipokuwa wakimkamata.
Jamaa wetu eti alikuwa amekwenda bungeni kuandamana kuwatetea wanamuziki Wakenya.
Mimi wala sina shida na ajenda aliyokuwa nayo sababu nishamchoka, ila alinichekesha sana kwenye tukio hilo. Wakati polisi wanang’ang’ana kumkamata, kwa bahati mbaya au nzuri sijui, mkono wa mmoja wao ukateleza na kutua kwenye paja.
Eeeh kumbe hata Eric ana paja mzee, kweli usidharau wembamba wa reli! Kule kuguswa kwenye paja, kulimtia mzuka jamaa. Akawa mkali hata kuliko wale polisi wenye rungu.
“Usinishike bana, usinishike mapaja, usinigay”…
Haya ndio maneno yaliyomtoka Eric. Aisee nilicheka sana ujue. Halafu kule Kamiti unaambiwa wahalifu sugu watatu waliamua kumwiga El-Chapo na wakafanikiwa.
Mlanguzi huyo maarufu wa dawa za kulevya amewahi kuhepa jela mara mbili. Mara ya kwanza alihepa 2001 baada ya kuwalipa pesa za kutosha walinzi.
Aliondolewa kwenye toroli la nguo chafu na akatoweka na kwenda kuendelea na biashara zake.
Alikamatwa tena miaka 14 baadaye na safari hii, alitoroka kupitia tundu la zaidi ya kilomita tano lililochimbwa kutoka nje na kuja kutokea kwenye bafu ya seli.
Aliingia kama vile anakwenda kuoga. Akateremka na ngazi alizokuwa amewekewa na wapambe wake. Kule chini kulikuwa na pikipiki, aliyoiwasha na kuyoyomea.
Hiyo ilikuwa ni kwao Mexico. Safari hii akiwa jela huko Marekani, wanasema ili aweze kutoroka tena, atahitaji msaada wa malaika.
Sasa na huku kwetu, magaidi watatu hatari walitoweka wiki hii kutoka gereza la Kamiti.
Hili ndilo gereza lenye ulinzi mkali zaidi kuliko yote nchini. Kwa wakati wowote ule, jela hili hulindwa na maafisa zaidi ya 100.
Aidha limezungukwa na ua mbili zenye urefu wa mita tatu. Katikati ya kuta hizo za ua huwa kuna maafisa wanaozunguka wakiwa juu ya farasi na pia mbwa wa kunusa.
Lakini katika mazingira ya kustaajabisha, wahalifu hao walifanikiwa kutoweka kwa kuruka ua hizo wakitumia kamba walizotengeneza kwa blanketi walizochana chana.
Isitoshe, Kamiti ina minara (watch tower) saba ambayo yote huwa na walinzi masaa yote 24.
Aisee!Ila drama iliyoniwacha hoi mimi ni ya binti Shirleen na mpenzi wake Kenneth Cabugah. Madogo hawa bwana waliinyorosha nchi vilivyo.
Shirleen mwenye umri wa miaka 20, alianza kwa kuposti stori ndefu kuhusu jinsi anavyohangaika na maisha baada ya kuzaa na kuachanishwa.
Lakini pia akadai jinsi alivyoweza kujizatiti na kuanzisha kundi la mademu kama wenzake ili kuweza kuwatembelea wenzao wanaopitia hali sawia wakiwapa misaada.
Haikuchukua muda kabla ya Wakenya kuanza kumchangia fedha.
Tatizo la Wakenya wengi na huruma yao, hawakugundua kuwa nambari waliyokuwa wakituma pesa ilikuwa na jina la Cabugah.
Fedha zilipofika laki 800, Cabugah akaanza kuwaringia mabestie wake. ‘Sasa nikinunua gari mpya kuna shida!’ Ila mmoja wa rafiki zake hao wenye wivu aliokuwa akiwaringia kwenye WhatsApp, akaamua kumwanika.
Fedha hizo sasa zimezuiliwa na M-Changa, mtandao uliokuwa ukitumiwa kuzichangisha. Nimeipenda akili ya Cabugah ya kutengeneza pesa bila jasho, lakini pia namcheka kwa namna alivyodharau nguvu za ‘karma’.
Tafadhali mchekini jamaa huenda alishazirai.