DOMO: Sista-du Avril, usanii ni kujitolea

DOMO: Sista-du Avril, usanii ni kujitolea

NA MWANAMIPASHO

JUZI Avril baada ya ukimya wa tuseme mwaka hivi au zaidi, aliachia ngoma yake mpya Danger kimya kimya.

Mimi ni mfuatiliaji mkubwa wa tasnia yetu ya burudani. Huwa najizatiti na kujitahidi sana kuhakikisha kuwa hamna linalonipita.

Ila sitaongopea, hii kazi mpya ya Avril mwenyewe sikujua kama inatoka lini. Nilishtukia tu ikijadiliwa kwenye blogu za udaku ndipo nikajua. Unapoona jambo likijadiliwa kwenye blogu za udaku, kuwa na uhakika hamna kizuri kinachozungumziwa.

Blogu hiyo ilipoposti skrinishoti ya wimbo huo kutoka kwenye chaneli yake Avril ya Youtube yenye zaidi ya Subscribers 100,000 amini usiamini, ilikuwa imetizamwa na watu 976 pekee ndani ya muda wa saa nane toka alipoachia.

Hadi naketi zangu kitako kuyatiririsha mawazo haya, ngoma hiyo ilikuwa ikipambana kufikisha angalau views 30,000. Kumbuka hiyo ni baada ya siku nne toka alipoachia.

Amini usiamini huyu tunayemzungumzia ni miongoni mwa wasanii wakubwa wazalendo watakaokumbukwa na historia kwenye tasnia ya muziki hasa wa kizazi kipya.

Huyu ni msanii ambaye Instagramu ana zaidi ya wafuasi milioni wanaofuatilia shughuli zake. Bado hujajumulisha na wale wa Facebook. Kwa hesabu za haraka Avril atakuwa anao zaidi ya watu 1.5 milioni wanaofuatilia maisha na kazi zake lakini bado walishindwa kumwonyesha upendo.

Kenye posti ile, kuna jamaa alishangaa vipi Wakenya tunashindwa kumpa mrembo wetu sapoti. Hapo akafungua uwanja wa mdahalo. Wengi ni waliomchamba bibiye, wachache wakamwonyesha upendo.

Waliomchamba wengi walihoji kuwa sista-do kachoka. Wengine wakamtambia kuwa muda wake wa kutesa umefikia mwisho bora arudi zake kwao Nakuru aone nini cha kufanya. Kama atafuga kuku wa mayai au auze nyanya sokoni sababu muziki kwake ndio basi tena. Sio Freshi barida tena.

Binafsi nilishindwa kabisa kumwonyesha upendo. Sio kwamba nina chuki naye, hapana. Ila kusita kwangu kuonyesha upendo ni kuhisi uzembe wa kutojituma.

Avril alikuwa anawaza nini kuachia muziki mpya baada ya kukaa kimya kwa zaidi ya mwaka, bila ya kuitangaza? Avril anaelewa kabisa maana ya biashara ni matangazo.

Muziki ni lazima usukumwe. Hata uwe staa ni lazima usukume kazi yako. Pengine alitegemea akishaposti Instagramu basi inatosha. Unaona matokeo sasa. Hata Diamond ambaye Avril ametangulia kuwa staa kabla yake, kila leo akiachia ngoma pamoja na ustaa wake, yeye hujitahidi sana kuisukuma.

Atasaka mahojiano na vyombo mbalimbali ilimuradi kutangaza ujio wake mpya. Ila shangazi kama vile hakujali. Aliona wadau watamkubali tu. Alisikia wapi?

Tumeshuhudia wasanii wakisukuma kazi zao hata zikiwa mbovu na bado zikafanya vizuri. Ingawaje chema chajiuza kwenye muziki hiyo haipo. Ni lazima uitangaze kazi yako. Sasa pana faida gani ya kuachia wimbo bila ya kupata faida yake. Ule mchecheto aliokuwa nao zamani wa kusukuma muziki wake ulienda wapi? Au ndio kweli kachoka na muziki? Nimeanza kuhisi hivyo.

Baada ya kuchambwa, Avril alitoa kauli akisema anachojua, ngoma zake zitatrendi atakapofariki. Sasa huu ndio mfano wa mbaazi ishindwapo kuzaa, husingizia jua.

Kazi zake za awali zilizofanya vizuri ni kwa sababu alizisukuma au alisukumiwa. Angalau hata jamani shangazi angeibua hata ka kiki, aichangamshe gemu tujue kweli karudi. Shauri yake bwana, anaelewa kabisa alijichanganya mwenyewe. Kama alitegemea ufuasi wake mkubwa mitandaoni ungepelekea mambo kuwa freshi barida, basi mpeni taarifa kutoka kwa rapa Khaligraph Jones, ‘Kuwa msanii Kenya ni kujitolea’ Lakini yeye, alijipotezea.

  • Tags

You can share this post!

Wasichana wa Kenya waendelea kung’aria wapinzani...

KASHESHE: Ezekiel Mutua arudisha ngori

T L