DOMO: Walichomea picha shangazi Riri!

DOMO: Walichomea picha shangazi Riri!

NA MWANAMIPASHO

IJUMAA iliyopita nilipata mwaliko wa kuhudhuria uzinduzi wa biashara ya Bi mkubwa BadGal Riri, Fenty Beauty pale The Social House, Nairobi.

Mwaliko huo ulitoka kwa kampuni ya Oby Africa yake Kagwe Mungai, iliyopewa dili ya kuandaa uzinduzi huo na Lintons Beauty, wakala watakaokuwa wakiuza mzigo huo wa shangazi Riri.

Bwana kwa kuwa mwaliko ulisema itakuwa ni hafla ya watu wachache yaani Exclusive, nikaamua lazima mtoto nitapendeza na kunukia vizuri. Huyo nikapitia pale kinyozi na kupigwa bonge la cut licha ya upara wangu ulioanza kuchungulia. Ndevu zangu pia zikatiwa nakshi nikaridhika sura itapendeza sababu ninajijua sina makunyanzi. Kisha nikaisindikiza sura hiyo ya pesa na suti moja hivi ya kizazi sasa na marashi ya S.T Dupont Perfect Tobacco. Mwana wee, nilikuwa nanukia zaidi ya waridi, uliza afisini watakwambia.

Saa moja unusu, huyo mimi nikatinga zangu Social House. Pale getini nikakutana na mabaunsa watano wenye suti nyeusi, wamezikunja nyuso zao kama jamaa ambaye kaenda haja kubwa halafu kwa bahati mbaya akawa hajakunywa maji. Si wajua jinsi shughuli hiyo huwa nzito mzee. Ningalikuwa na kitisheti walai wangenidhalilisha ila ule mwonekano wangu kidogo uliwafanya hao magoliath na sura zao ngumu kama kesi ya shamba, kuny’ong’onyea.

Yule binti mhudumu akalitafuta jina langu na kunipa tiketi nyeupe. Kabla sijaondoka akafika mwigizaji staa ambaye ni swahiba wangu, yeye akapewa tiketi nyeusi. Duh! Ikanisumbua ishu hiyo hadi pale nilipomsikia binti mhudumu akimnong’onezea, “baada ya shughuli pitia nina zawadi yako utaipenda‚Ķ” Mzee baba hapo ndio nikagutuka kumbe nipo kwenye hafla ya kibaguzi sababu nilipouliza kama na mimi nitapata zawadi, dada huyo aliniambia, zawadi ni za watu wenye tiketi nyeusi tu.

Nikaona isiwe kesi, nikaongozwa kwenye lifti na kujikuta kwenye orofa ya tano ilikokuwa ikifanyika shughuli yenyewe. Aisee! kusema la kweli moyoni, kwa shughuli nyingi za uzinduzi nilizowahi kuhudhuria, sikutegemea kuwa ile ya Riri ingekuwa vile. Nilitegemea kupata tukio la Red Carpet, ila niliishia kukutana na sura zingine ngumu za mabaunsa wawili. Baya hata zaidi, hawakuwepo wapambe wa kuwaeleza watu programu ya siku.

Isitoshe, sehemu yenyewe ilikuwa ndogo mno. Katikati kulikuwepo na baa ya wazi (open bar). Kushoto kulikuwepo na ukumbi wa kujistarehesha wa watu kama 50 hivi halafu kulia ilikuwepo kama soko la wauza nyanya vile. Wanawake kule walikuwa wanapambania kupakwa vipodozi vya Fenty sababu ilikuwa ni ofa ya bure. Mwenyewe nikawa nashangaa, make-up unapakwa usiku ukienda wapi? Lakini tena si uzinduzi wa mzigo wa shangazi Riri halafu ulivyo na bei, nani asingependa kujitesti? Kisha si wajua vya bure havina mwenyewe?

Mpaka sasa yote haya nimebaini kwa kuulizia ulizia niliowakuta pale kuhusu kinachoendelea. Sikutegemea ungekuwa uzinduzi wa mtu kujikanganya. Kutokana na eneo kuwa dogo, nilitegemea wageni waalikwa watakuwa wachache, si ndio maana ya Exclusive. Lakini kadri muda ulivyozidi kwenda ndivyo chumba kilizidi kufurika na kila aina ya celeb umjuae.

Nilisubiri kusikia mwandalizi akitoa hata maelezo ya programu lakini wapi. Tulikuwa tupo sokoni kila mmoja ajihangaikie. Basi mimi nikaamua kukesha kwa kuitisha vinywaji sababu vilikuwa vya bure na pili kwa sababu sikuwa najua kilichokuwa kikiendelea. Kufika saa tano usiku chumba kilikuwa kimefurika na maceleb kibao mpaka kina Crazy Kennar, nikawa nashangaa alialikwa kuja kufanyaje jamani.

Baya hata zaidi, mwaliko haukutupa aina ya vazi rasmi hivyo kila mmoja alikuja kavaa alichotaka yeye. Ndio sababu wengi waliishia kuchambwa mitandaoni kwa kuchagua mavazi yaliyokosa kuendana na tukio. Ila mliwalaumu na kuwashtumu wakati lawama ilipaswa kuwa ya waandalizi. Hata Bensoul alifika na tisheti ya kulala kwa mtazamo wangu. Mmoja wa wakurugenzi wa Lintons naye alifika amevaa fuaa, utadhani halikuwa tukio la maana.

Saa sita wakati watu wakiwa wameshalewa ndio binti mmoja alijaribu kusoma hotuba ya uzinduzi. Hakuna aliyemsikia. Kipaza sauti kilifeli lakini pili watu walikuwa wameshalewa na kuchoka kwa kukesha wakibung’aa na kupiga mastori wasijue kilichokuwa kikiendelea. Ilikuwa ni hafla ya kipuzi, ya kitoto ya kuabisha kwa brandi ya shangazi Riri. Waandalizi walichoma sio tu picha, walichoma hadi na vyeti kwa uzinduzi feki na ovyo. Kilichoniuma hata zaidi ni pale wenye tiketi nyeusi walichukuliwa na kupelekwa kupiga sherehe Club Gemini. Sisi kina yakhe wenye tiketi nyeupe, tukaambiwa, ‘Asanteni kwa kuja’. Wakwende ‘uko. Bure Kabisa!

You can share this post!

KIPWANI: Kaingiza zigo la mwisho sokoni

BrighterMonday yazindua teknolojia ya kuwasaidia waajiri...

T L