Bambika

DOMOKAYA: Hivi kweli haya mapenzi yana maana gani haswa? Binadamu hapendeki!

March 1st, 2024 2 min read

NA MWANAMIPASHO

Duh! Hivi wanazengo hebu soogeni karibu niwaulize jambo. Hivi kweli haya mapenzi yana maana?

Maana mimi binafsi sioni. Bwana binadamu hawapendeki. Kheri umpende mbuzi maana utakuja kufaidi mchuzi, ila binadamu, utaishia kudharauliwa na kuteseka mtima.

Juzi mumeona jinsi Zuchu alivyolia Insta kwa machungu akisema amechoka na dharau za Diamond baada ya msela kuposti video ya kichokozi na mama watoto wake soshiolaiti Zari Hassan.

Lakini dada baadaye alizenguliwa kwa kuombwa msamaha na akarudi boksi ya Simba la Masimba. Kumbuka hili sio tukio la kwanza la dharau kwa Zuchu. Kuna pia lile tukio kwenye Young, African Rich and Famous ambapo Diamond alikula ubuyu wa Fantana yule dada kutoka Ghana.

Zuchu baadaye alikiri kuvunja vikombe na masahani nyumbani kwake Diamond baada ya kutizama ile Reality Show na tukio hilo.

Mwanzo kabisa pamoja na kwamba Zuchu anaamini kwenye penzi, sijui aliona wapi kwamba kunguru anafugika. Habari zote anazo kuhusu mienendo ya Diamond maana wameshapita madem wengi kabla yake na wengi wameumizwa.

Sasa yeye kuendelea kuwa king’ang’anizi ndio jambo linanifanya kushindwa kuelewa kama haya mapenzi yana maana kweli kama tu alivyowahi kuimba huyo Diamond kwenye ngoma yake ya Mapenzi Basi.

Lakini vile vile kuijenga picha hii hata zaidi, kuna stori hii ya Lupita Nyong’o juzi kaulizwa kwa nini aliweka wazi penzi lake na Selema Masekela na baada ya kitumbua kuingia mchanga akaamua kuweka wazi vile vile.

Kabla ya Selema, Lupita hakuwahi kuweka mahusiano yake wazi.

Kwenye majibu yake, Lupita alikiri kwamba aliamini kabisa penzi lake na Selema lingefika mbali. Kwamba alikuwa na uhakika wa hilo jambo na ndio maana akasadikika kuitangazia dunia. Lakini hata baada yake kuumizwa kama alivyoumizwa, bado kama tu Zuchu, Lupita anazidi kugangamala kwenye penzi.

Anasisitiza kuwa lengo kubwa la binadamu duniani ni kusaka penzi. Kwa hiyo hatachoka kusaka penzi tena.

Jamani eeh! Hebu niambieni kama kweli haya mapenzi yana maana maana hata mimi mwenyewe yangu yamenishinda na nafikiri bora kukaa tu kibwege bwege. Kheri amani hiyo au?