DONDOO: Madugu wageuka mbwa na paka

DONDOO: Madugu wageuka mbwa na paka

Na Nicholas Cheruiyot

Mwanasiasa limbukeni alivunjika moyo mpango wake wa kumhamisha nduguye kwake ili amuachie boma atumie kujipigia debe ulipogonga mwamba.

Duru zinasema jamaa huyo amekuwa akifanya kazi katika mji wa mbali na huishi huko na familia.

Majuzi, jamaa aliamua kujirusha katika uwanja wa kisiasa na maadamu hana nyumba ushago, alimwomba ndugu yake ampishe kwa kukubali ampangishie nyumba katika mtaa mmoja eneo hili naye ahamie boma lake hadi anyakue kiti.

‘Ndugu, kilio cha raia cha kunitaka niwahudumie kama kiongozi kimezidi na sina budi ila kuitikia wito. Shida ni kuwa sina nyumba huku na huenda wapinzani wakanitaja kama mgeni,’ jamaa alimwambia ndugu yake.

‘Kwa hivyo unataka nikusaidie vipi? Si ujenge hata kibanda cha kushikilia?’ kaka yake alimhoji jamaa.

‘Mheshimiwa mtarajiwa hawezi kuishi kibandani. Ninataka nyumba kubwa kama hii yako. Ninataka nikupangishie nyumba mtaani hadi niwe mheshimiwa mwaka ujao ili nianze kujenga yangu ya kifahari,’ jamaa akamlilia kakake.

Inasemekana kaka alimpa kibali kufanya hivyo kwa masharti kuwa akichaguliwa atamsaidia kwa ukarimu wa hali ya juu.

‘Majuzi, jamaa alifika ushago akiwa ndani ya lori lililokuwa limejaa vitu, vingine vikining’inia kwa kukosa nafasi. Pindi lori lilipoegeshwa, mushkili ulitokea mke wa ndugu yake alipopinga vikali wazo la kuhamishwa,’ mdaku akasimulia.

‘Siwezi kamwe kukuacha udandie kwangu nikihangaika mtaani. Nendeni kuishi katika mtaa, sibanduki huku,’ mrembo alishikilia na jamaa akajipata kona mbaya na akaamua kwenda kukodisha chumba mtaani akiwazia hatua ya kuchukua.

 

You can share this post!

Bila kuzingatia muktadha, neno ‘hakika’ halipaswi...

CHAKISE; Nuru inayovumisha mawimbi ya Kiswahili Shuleni...