Dondoo

DONDOO: Mdogo kazini afutwa kazi akibishania mwanamke na mkubwa wake

January 22nd, 2024 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

Polo mmoja kutoka mashinani ya eneo la Kati amefutwa kazi baada ya kupigania mahaba ya mwanamke na mdosi wake.

Duru za wadokezi zinasema kwamba mdosi huyo alikuwa akimnyemelea mwanamke fulani mtaani huku naye mdogo wake akiwa na ajenda kwa mzinga uo huo.

“Shida ilitokea hivi majuzi katika hafla moja mtaani Nyeri ambapo mdosi na mdogo wake walihudhuria na kukawa na mvinyo. Kwa upande mwingine, yule mwanamke wa kutesa nyoyo zao akafika,” mdokezi akakariri.

Huku mdosi na mdogo wake wakizidi kujipa mvinyo na ulevi ukawakamata vizuri, walianza kumsaka yule mwanamke kwa nia ya mahaba.

“Walikutana wawili mbele ya huyo mwanamke na shida ikatokea. Balaa kubwa ambapo polo mdogo wa mdosi alitoa maneno ya kukosea mamlaka heshima,” akasema mdokezi.

Ilifika mahali ambapo mkubwa na mdogo wakiwa ndani ya ulevi wao nusura washikane mashati lakini walevi wengine wakawashinikiza kuweka amani.

“Lakini mdosi alisikika akiapa kwamba ni lazima angemtia mdogo wake adabu za afisi na kwa uhakika, polo hayuko kazini huku yule mwanamke akiwa sasa ni mali ya mdosi,” mdokezi wetu akasema.

Sasa, imekuwa sheria katika hiyo afisi kwamba ukimwona mdosi ananyemelea, kaa mbali la sivyo ujipate nje ya ajira.

[email protected]