Dondoo

DONDOO: Mume afumaniwa na mkewe bafuni akiwa na kimada

January 31st, 2024 1 min read

MATENDENI, EMBU

NA JOHN MUSYOKI

MWANAMUME alitamani ardhi ipasuke apotelee ndani, mkewe alipomfumania akiwa bafuni na mpango wake wa kando wakioga.

Duru zinasema jamaa alikuwa na tabia ya kualika mpenzi wake wa pembeni mkewe akiondoka kwa shughuli zake za kibiashara.

Laki siku ya arubaini ilitimia, jamaa alipoalika kimada wake na wakaanza burudani ilivyokuwa desturi. Baada ya wawili hao kurushana roho na kuchoka waliingia bafuni kuoga kwa bashasha huku wakiangua vicheko.

Mkewe aliyekuwa amefahamishwa kuhusu tabia yao alifika na kubisha mlango wa bafu kwa fujo huku akitishia kuvunja mlango lakini jamaa akaufungua na kuchomoka akiwa amejifunika taulo.

Naye mpango wa kando wake alijikunyata kwenye kona kama kuku aliyenyeshewa. Mke wa jamaa aliondoka baada ya kuthibitisha kweli mumewe alikuwa mzinifu.

***

Shambaboi akataa agizo la bosi kuchunguza mke

ITHANGA, MURANG’A

NA JOHN MUSYOKI

SHAMBA boi wa hapa alimzima mdosi wake kwa kumtaka awe akimchunga mkewe asije akanyemelewa na wanaume wengine kijijini.

“Kuanzia leo nataka uwe unamchunguza mke wangu. Ukijua ana mpango wa kando uniambie.” Nitakuongezea mshahara mradi utanisaidia kupata fisi anayenyemelea mke wangu,” akasisitiza.

Hata hivyo, jamaa alimzima mdosi wake vikali akimwambia ajichunguzie mwenyewe ikiwa hamwamini mkewe.

***

Jombi mkono gamu ahepwa na vidosho

DIANI, KWALE

Na JANET KAVUNGA

POLO mmoja wa hapa alishtuka mwanadada aliyemrushia mistari ya mapenzi alipomwambia akome kujisumbua akisaka vidosho kwa kuwa anajulikana kwa kuwa mkono birika.

Jamaa amekuwa akitemwa na kukataliwa na vipusa wanapogundua kuwa hawezi kuwapa pesa. Juzi alimtongoza demu na akashangaa kuwa mademu wanajua ni mkono gamu.

“Usijisumbue kutongoza wasichana hapa mtaani kwa kuwa kila mmoja anajua hauwezi kununua hata chupa ya soda,” demu alimsuta jamaa.