Dondoo

DONDOO ZA HAPA NA PALE: Deti na binti ya bosi yamletea balaa

June 8th, 2019 1 min read

NA TOBBIE WEKESA

MAKONGENI, THIKA

POLO aliyekuwa akifanya kazi mtaani hapa alipigwa kalamu baada ya kupatikana baa akiwa na binti ya mdosi wake wakilewa.

Inasemekana polo alipatikana na mdosi wake mwenyewe katika baa moja maarufu eneo hili na akafutwa kazi papo hapo.

Kulingana na mdokezi, polo alikuwa dereva na kazi yake kuu ilikuwa ni kumpeleka mdosi wake alikokuwa akitaka.

Inasemekana mdosi alikuwa na binti ambaye alikuwa akimkosesha polo usingizi na jamaa akaanza kuweka mikakati ya kumnasa binti yule.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kumpata mrembo kwani aliogopa sana babake.

Duru zinaarifu kwamba polo na mrembo walikubaliana kukutana pahali salama mbali na boma lao wasije wakapatikana ili wajadili namna ya kuendesha penzi lao.

Penyenye zinasema mdosi wa polo alianza kuona binti yake akiwa na tabia ya kuongea kwa simu sana na akashuku huenda alikuwa akiwasiliana na dereva wake.

Duru zinasema siku ya tukio, polo alimpeleka mdosi kazini na baada ya muda mfupi alimuomba ruhusa akimbie nyumbani kusuluhisha jambo la dharura.

Kutafuta chamcha

Baada ya polo kuondoka, mdosi aliamua kuondoka afisini ili atafute chamcha.

Inadaiwa alishangaa kuona gari lake nje ya baa moja mkabala na hoteli aliyokuwa akienda kula.

Alipoingia ndani alipigwa na butwaa kumpata jamaa na binti yake.

“Sikujua kuwa una tabia hii. Kwangu usikanyage tena. Shetani wewe,” mdosi alimfokea polo.

Shughuli zote kwa baa zilisimama.

“Hili ndilo jambo la dharura uliloniambia unakuja kusuluhisha. Huna aibu hata kidogo kuketi hapa na binti yangu mapema hii kumnunulia pombe,” mdosi alizidi kumkaripia polo.

Polo alichomoka mbio lakini mbio zake hazikumfikisha mbali kwani alifuatwa na mabaunza ili alipie pombe waliyokuwa wamekunywa.

“Nimesema usiwahi kunipigia simu tena. Tafuta kazi kwingine. Umekuwa dudu liumalo,” mdosi alimzomea polo na kumpokonya ufunguo wa gari na kuondoka.