Dondoo

Mama akaanga vipusa kuhusu gumzo chafu

March 16th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

Huu hapa mkusanyiko wa visa na visanga vya kukuvunja mbavu:

 

Mama akaanga vipusa kuhusu gumzo chafu

TUWATUGAWE, MOMBASA

MABINTI wawili mtaani hapa walijipata pabaya baada ya mama yao kuwafumania wakijadili mbinu za kurushana roho na wapenzi wao.

“Mama alikuwa msalani alipowasikia binti zake wakijadili mbinu za kuwafurahisha washikaji wao,” asema mdaku wetu.

Mabinti hawakujua mama alikuwa chooni, walipoanza kushauriana jinsi ya kuwadekeza wapenzi wao.

“Nikimpata wangu kesho nitamuonyesha mapenzi mazito anichotee kiasi chochote ninachohitaji. Hata kama ni kumtumbuiza kitandani niko tayari,” binti mmoja alisikika akimwambia mwenzake.

“Wangu nitampeleka beach tukamalizanie huko, nikirudi sirudi bure,” binti wa pili alimwelezea mwenzake.

Mama yao akiwa chooni alisikia yaliyozungumzwa hadi akakatiza haja yake, akafungua mlango na kutoka nje ghafla.

“Endeleeni na gumzo lenu chafu, napoteza hela kuwasomesheni kumbe nasomesha makahaba hatari wachumao pesa kwa wanaume,” mama alifoka akiwakodolea macho mabinti.

Inasemekana vipusa hao walianza kusuasua, mama akaokota fimbo na kuwatwanga.

“ Nyinyi hamna adabu, sijui niliwazaa wa nini, hata hamna tabia kabisa,” mama aliwafokea huku akiendelea kuwacharaza kwa fujo.

Baba aliposikia mabinti wakilia, alitoka ndani ya nyumba akamwona mama akiwacharaza.

“Wuuii, usiniulie wanangu, wamefanyaje hadi unawaadhibu namna hii,” mzee aliropokwa kwa hasira.

“Waulize kinachofanya niwaadhibu, nilidhani nimezaa watoto kumbe nimezaa Malaya,” mama alimweleza mzee.

“Mbona sikuelewi, hasira za nini mpaka unaita wanao malaya,” mzee alitaka jibu lakini mama aliwataka mabinti wamjibu.
Hatimaye mzee aligundua mabinti walikuwa wahanyaji mtaani.

“Walishindwa kuelezea kilichosababisha waadhibiwe, hali iliyomfanya pia mzee kupandwa na hasira za mkizi na kuwaadhibu mara ya pili,” aliarifu mdaku. – Na Ludovick Mbogholi

 

Bwanyenye amtorosha mke wa pasta wake

VOI MJINI

Pasta wa kanisa moja mjini hapa aliangua kilio baada ya kupokonywa mke na bwanyenye aliyejiunga na kanisa lake majuzi.

Kulingana na mdokezi, bwanyenye huyo ni mfanyabiashara mtajika.

Alipofika kanisani, pasta alifurahia sana na akajua fika kuwa fungu la kumi lingeongezeka.

Kile ambacho pasta hakufahamu ni kwamba, jamaa alikuwa na uhusiano na mkewe.

Yasemekana mke wa pasta alianza kumdharau mumewe huku akiondoka na kurudi nyumbani na bidhaa za bei ghali.

Baada ya pasta kugundua, alimuuliza mkewe ambaye alijifanya hakuwa na habari kabisa.

Mumewe alipotisha kumpiga, mwanadada alipasua mbarika.

“Unashinda hapa ukiniuliza maswali ambayo uko na majibu. Ndio nimepata mwenye pesa na sina haja na senti zako. – Na Holiness Mwambi

WAZO BONZO

Wazo Bonzo Machi 16, 2019

 

Mama atelekeza wanawe kikaoni

MATUNGWA, MAKUENI

Mzee wa hapa alijipata pabaya mkewe alipomletea watoto kwenye kikao cha wazee.

Yasemekana mzee alitumia pesa za kulipia watoto karo kushiriki kamari huku akinuia kupata donge nono.Wawili hao walianza kuzozana watoto walipofukuzwa shuleni mzee alipoitishwa pesa na kusema alikuwa amezitumia.

Baada ya siku tatu, mkewe alikasirishwa na tabia hiyo na akaamua kumpelekea mumewe watoto kikaoni.

Wazee tayari walikuwa wamezama kwenye gumzo huku wakijadili masuala yao.

Mzee aliona haya kumuona mkewe akiandamana na watoto.

Mama alianza kumfokea mzee akimlaumu kwa kutumia pesa walizokuwa wamehifadhi.

Jaribio la kumzima mkewe halikufua dafu.Mke alitikisa kichwa na kumuachia watoto. – Na Mirriam Mutunga

 

Kioja polo kuponea bakora ya kalameni

RHONDA, NAKURU

Jombi mmoja mtaani hapa, aliacha kusonga sembe na kutorokea dirishani alipopata fununu kuwa mzee wa mtaa alikuwa akimsaka.

Inasemekana jamaa alikuwa miongoni mwa kundi la vijana waliomtukana binti ya mzee wa mtaa jioni moja akitoka saluni.

“Jamaa na wenzake walikuwa wakichana veve, mrembo alipowapita bila kuwapa salamu. Stimu zilipanda kichwani wakaanza kurusha cheche za matusi, wakimtaka mwanadada aache maringo na ajifundishe kukaa na watu,” aliarifu mdaku.

Alipokuwa akipika sembe kwake alisikia mzee wa mtaa akiteta nje na akajua mambo yalikuwa mabaya. Alizima stovu na kutorokea dirishani kwenda mafichoni.

Duru zasema mzee bado amsaka kwa lengo la kumkamata jamaa kwa kudunisha binti yake mrembo. – Na Richard Maosi

 

VITUKO VYA POKOYOYO

Vituko vya Pokoyoyo Machi 16, 2019