Dondoo

Polo aambia kanisa babake ni tapeli

March 30th, 2019 2 min read

SOY, UASIN GISHU

JOMBI wa hapa aliwashangaza waumini wa kanisa kwa kuwaambia kwamba baba yake alikuwa pasta tapeli.

Jamaa aliwaarifu washirika kwamba baba yake alikuwa akiwapotosha. Inasemekana baba ya jamaa alirejea hapa kutoka jijini na kisha akaanzisha kanisa.

Kwa muda mfupi, kanisa hilo lilianza kuwa na waumini wengi hata kushinda makanisa mengine.

Hata hivyo, jamaa alidai babake alikuwa na kesi nyingi zinazohusiana na utapeli.

Alidai kwamba babake alifukuzwa kutoka jijini Nairobi baada ya kutapeli mwanamume mmoja Sh150,000.

Jamaa alisikitika kwamba, washiriki walikuwa wamepumbazwa macho kuamini kwamba walikuwa wakipokea uponyaji bila kujua lengo la baba yake ni kuwatapeli.

“Nataka kuwaambia kitu ambacho hamjui. Huenda mtashtuka lakini mjue ni ukweli wa mambo. Mkitaka mnichukie, mkitaka msiniamini lakini nitakuwa nimewaambia. Babangu si mchungaji halali. Ni tapeli mkubwa sana,” alisema kijana.

Kanisa lilibaki kwenye mshangao wasiamini maneno hayo. Polo aliwatolea mifano ya jinsi hela za kanisa hilo zilikuwa zikipotea kwa njia tatanishi. Baadhi yao walidai kwamba huenda kijana huyo alikuwa akitumiwa na mahasidi wa kanisa hilo huku wengine wakisema huenda alikuwa akisema ukweli.

Wakati wa kisa hicho, baba ya jamaa hakuwa kanisani.

Polo alidai alikuwa amekosana na babake mara kwa mara kutokana na msimamo usiotetereka wa kusema ukweli.

“Mjue kinachofanya nitofautiane na baba yangu ni kwamba, napenda ukweli. Nilipomkosoa kwa kwenda kombo, alidai mimi ni mtoto mbaya,’’aliongezea jamaa.

Wazee wa kanisa waliapa kufanya uchunguzi kuhusu madai ya jamaa huku akiwashauri washiriki kutohama kanisa
hilo. “Hakuna haja ya kuhama. Ngojeni ukweli utajulikana,’’alisema mwenyekiti wa kamati ya wazee kanisani. – Na DENNIS SINYO

Nani hapa anasema ukweli?

 

Pasta atekwa na mama sukari na kutema familia

MWANDA, TAITA

WAUMINI wa kanisa moja eneo hili walipigwa na butwaa kugundua kwamba pasta wao alikuwa ametekwa na mama sukari hadi akateleleza familia yake.

Ripoti ziliarifu kuwa, mama huyo alijiunga na kanisa hivi majuzi.

Kila mara alikuwa akitoa sadaka kubwa na fungu la kumi pamoja na kufadhili miradi tofauti kanisani.

Alianza kumchangamkia kwa kumnunulia chamcha kila Jumapili na kila wakati pasta alipokuwa akienda safari, alikuwa akijitolea kumpeleka kwa gari lake.

Akidhani ni miujiza iliyokuwa imetendeka, pasta alianza kuwa karibu na mama huyo na kila jioni mama alimwalika nyumbani kwake kwa kikombe cha chai na maombi.

Pasta alianza hata kulala kwa mama huyo na kurejea kwake asubuhi na mkewe anapomuuliza alimweleza alichelewa kwa huduma. – Na HOLINESS MWAMBI

 

WAZO BONZO

Wazo Bonzo, Jumamosi, Machi 30, 2019

Kiu ya kileo yamtupa mashakani kilabuni

MAKIMA, MWEA

JAMAA mmoja kutoka hapa alinusurika kichapo kutoka kwa mapolo kilabuni kwa kuteremsha pombe ya demu.
Kulingana na penyenye, jamaa alichukua chupa ya pombe ya mwanadada huyo baada ya kukosa mtu wa kumnunulia dozi.

Demu alipiga kamsa jamaa alipochukua pombe yake na kuvutia waliokuwa kilabuni.

Kitendo cha jamaa huyo kiliwakera wahudumu na wateja na wakaamua kumfunza adabu.

Watu walimrukia huku kila mmoja akitaka kumtwanga lakini kwa bahati, walinzi wa kilabu hicho waliingilia kati na kumuokoa.

Licha ya jamaa kunusurika kichapo hicho, watu walimrushia kila aina ya maneno.

“Wewe ni mwanamume sampuli gani,” watu walifoka kilabuni.

Inasemekana demu alinunuliwa pombe na wanaume kadhaa huku jamaa akitoroka. – Na JOHN MUSYOKI

 

Wazazi vinywa wazi polo kutema mkewe

NYAMARANGA, MIGORI

JAMAA mmoja kutoka hapa aliwashangaza wengi alipodai kwamba amechoka kuishi na mkewe.

Inasemekana polo alimtaka mkewe arudi kwao ili ampe nafasi ya kurejelea maisha yake ya hapo awali ya ukapera, maisha aliyodai hayana vikwazo vyovyote.
Kulingana na mdokezi, polo aliwaomba wazazi wake wamsihi kipusa arudi kwao, la sivyo atamlazimisha kufanya hivyo.
“Namtaka huyu mwanamke arudi kwao. Nimechoka kuishi naye,” polo alidai. Inadaiwa wazazi wa polo walibaki midomo wazi wasijue la kufanya.
“Nilipokuwa kapera, nilikuwa na uhuru mwingi sana. Leo hii siwezi kufanya jambo lolote bila ruhusa yake. Heri aende,” polo alisema. – Na TOBBIE WEKESA