• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 5:46 PM
Arudi na zawadi alipokosa mlo harusini

Arudi na zawadi alipokosa mlo harusini

Na LEAH MAKENA

KEROKA, Kisii

MAMA wa hapa alishangaza wengi alipokataa kupeana zawadi kwa maharusi na kurejea nayo nyumbani kwake kwa kukosa pilau shereheni.

Habari zasema kuwa mama alikuwa jirani ya binti aliyekuwa na harusi, na alikuwa akihudhuria mikutano ya harambee na kuchangia pakubwa kufanikisha harusi hiyo kando na kununua zawadi ya sufuria mbili alizobeba ili kukabidhi wanandoa.

Sherehe iliendelea ilivyotarajiwa hadi jioni waliohudhuria walipoagizwa kujipanga ili wapate chakula.

Inasemekana kuwa mama alikataa kufuata utaratibu na kujiunga na upande wa wazazi akisema kwamba alikuwa mtu wa maana kwa kidosho.

Hakuamini kwani wapishi walikataa kumpa chakula na kushikilia kuwa walikuwa wanajua wazazi na hivyo kumtaka mama kufuata utaratibu uliotumiwa na wengine kupata chakula.

“Tulikuwa tumeonyeshwa wazazi wa pande zote mbili na hao pekee ndio wanatumia meza spesheli. Hao wengine wanapewa chakula kutoka upande wa pili. Hatutaki msongamano upande huu kwa sababu ni muhimu kuheshimu wazazi wa maharusi,” mmoja wa wapishi alieleza.

Licha ya kuelezewa alivyostahili kufanya, mama aliendelea kuvutana na wapishi kwa dakika kadha na kuwafanya kuondoka walipomaliza shughuli yao.

Hapo ndipo alifululiza upande wa pili lakini akaambulia patupu kwani alipata chakula kilikuwa kimeisha. Hakufanikiwa kupata chochote kwani wapishi walimfungulia sufuria tupu na kumueleza jinsi walivyoruhusu watu kuchukua chakula hata mara mbili.

Mama alipandwa na mori na kuamua kuanza safari ya kurejea kwake mapema huku akihepa shughuli iliyokuwa ya mwisho ya kutoa zawadi.

“Kwa nini nitoe zawadi na nimebaki nikiwa njaa pekee yangu? Sasa nimepata matokeo ya kujishughulisha kwa muda mrefu kwani hata niliowashughulikia leo hawanitambui. Nitatumia sufuria kupikia kwangu, hata sikuwa na za kutosha jikoni,” mama alisema na kuondoka.

You can share this post!

Jamaa wa Gumo aliyetekwa nyara aachiliwa

TAHARIRI: Kampeni ghali ndizo zinazotuchongea

T L