• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Atumia kahaba kuzima polo msumbufu

Atumia kahaba kuzima polo msumbufu

Na JOHN MUSYOKI

MATUU, MACHAKOS

KIOJA kilishuhudiwa katika ploti moja mtaani hapa, jamaa alipopiga nduru baada ya mama aliyetarajia kuburudika naye kutuma vipusa wawili chumbani wamrambishe asali.

Duru zinasema jamaa alikuwa akimtongoza mama wa umri mkubwa ambaye ni mke wa mtu. Mama aliamua kumkomesha na kumpa miadi wakutane katika chumba chake.

Duru zinasema mama alimtafutia vipusa wawili na kuwalipa wampangawishe jamaa ili akome kumnyemelea.

“Usiwe na wasiwasi. Hata nikikosa chumbani utapata watu wa kukukaribisha,” mama alimwambia polo kwenye simu.

Yadaiwa jamaa alifika chumbani kwa bashasha za kila aina. Alikuwa ameng’ara kweli kweli. Alipobisha mlangoni alikaribishwa na vipusa wawili waliojikwatua kwatu kwatu.

Vicheko vilisheheni chumbani huku vipusa hao wakimchangamkia jamaa.

Inasemekana vipusa walianza kumpandisha jamaa mzuka. Walimkonyozea macho, kumpapasa huku wakimvua shati.

“Nini inaendelea hapa? Yuko wapi mwenye nyumba? Hebu acheni hizo!’ jamaa alilalamika.

“Acha kujifanya mjinga. Haja ya kuja hapa ilikuwa ni nini? Aliyekuita hapa hayuko na alitupatia jukumu la kukuhudumia,” kipusa mmoja alisema.

Inasemekana jamaa alianza kupiga nduru huku akijaribu kujinasua mikononi mwa kina dada hao.

“Jamani! Niacheni. Njooni mniokoe. Hapana. Mimi sitaki,” jamaa aliteta.

Katika vuta n’kuvute hizo, mama alifika na kumpata polo akipambana kujinasua.

“Nini kinaendelea hapa? Yaani umeshindwa kufanya kazi na vile ulikuwa unajishasha eti wewe ni gwiji wa uroda! Kama umeshindwa na warembo hawa mimi huniwezi,” mama alisema.

Ilibidi jamaa kuangua kilio alipogundua vipusa hao walikuwa makahaba.

Jamaa alifukuzwa kama mbwa koko.

“Kwenda kabisa. Wewe ni mtu bure kabisa,” mama alifoka.

Inasemekana baada ya kisanga hicho polo aliacha kumtongoza mama huyo.

You can share this post!

Niko tayari kumenyana na mradi wa Uhuru, Ruto asema

Kocha wa Leopards atosheka na jinsi vijana walivyocheza

T L