• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 5:30 PM
DONDOO: Barobaro akemea ‘mumama’ aliyejaribu kumrushia ndoano ya mapenzi

DONDOO: Barobaro akemea ‘mumama’ aliyejaribu kumrushia ndoano ya mapenzi

MALINDI MJINI

Na JANET KAVUNGA

BAROBARO wa hapa alimkemea mumama mmoja kwa kumrushia mistari ya mapenzi licha ya umri wake kuzidi wa mama yake.

Jamaa ambaye ni meneja katika hoteli moja ya kitalii mjini hapa alichoshwa na jumbe za mara kwa mara kutoka kwa mama huyo akimweleza anavyomtamani.

Juzi, jamaa aliamua kumkomesha mumama huyo na akamkabili mbele ya watu alipomuita mpenzi wake.

“Nani unaita mpenzi wako. Nikome kabisa. Mimi ni sawa na mjukuu wako na siwezi kushiriki mapenzi na wewe. Sahau na uache kunitumia jumbe za mapenzi,” jamaa aliwakia mama ambaye alimwangalia tu na kutabasamu.

“Mwanamume ni kujieleza na umefanya hivyo. Hii ndiyo sababu sitaacha kukupenda,” mama alisema na kushangaza watu lakini jamaa akaondoka na kwenda zake.

***

EMBU MJINI

Demu atema polo baada ya kununuliwa simu

NA JOHN MUSYOKI

KALAMENI mmoja aliyemnunulia demu simu ya bei ghali akitamami wawe wapenzi alijuta baada ya kuachwa na demu kwenye mataa.

Demu alijifanya kumpenda jamaa kwa dhati ili atunzwe vizuri. Jamaa alijipendekeza kwa kipusa kwa kumnunulia simu ya bei ghali.

Inasemekana jamaa aliposisitiza kukutana na demu baada ya kupata simu, mwanadada alimtumia ujumbe kumfahamisha alikuwa na mpenzi mwingine na hakuwa chaguo lake.

“Najua itakuuma sana lakini ningependa kukufahamisha siwezi kuwa mpenzi wake. Asante kwa muda wako katika maisha yangu.

Nina mpenzi ninayempenda sana na ndiye atakayenioa. Asante kwa mazuri uliyonitendea na Mungu atakubariki na mwanamke mwema,” mwanadada alimwambia jamaa kwenye arafa.

***

Azima sherehe ya mwanawe kwa kushuku mke wake anachepuka

TEMBWO, SOTIK

NA NICHOLAS CHERUIYOT

POLO wa hapa alifutilia mbali sherehe ya kufurahia kuzaliwa mwanawe alipopata fununu kuwa huenda yeye si baba halali wa malaika huyo.

Inaarifiwa kuwa pindi tu walipojaliwa mwana, polo alitangaza mtandaoni habari hizo njema na baadaye akapanga siku ya kusherehekea pamoja na jamaa na marafiki.

Hata hivyo, sherehe ilipokuwa ikiwadia polo alipekua simu ya mkewe na kushangaa kuwa kuna jamaa mwingine aliyekuwa akiramba asali kutoka kwa mzinga aliodhani ni wake peke yake.

“Alihuzunika na kuwataka jamaa na marafiki kutofika kwake hadi abaini ukweli wa mambo,” mdaku aliarifu.

***

Mke alalamika meidi anavuruga ndoa yake

NYALI MJINI

Na JANET KAVUNGA

MWANADADA wa hapa alilalamika kuwa ndoa yake ilikosa amani tangu alipoajiri yaya wa kumsaidia kulea mtoto na kazi za nyumbani.

Demu alisema kabla ya kuajiri yaya, uhusiano wake na mumewe ulikuwa mzuri.

“Nashuku mume wangu anatafuna yaya huyo kwa sababu huwa hataki nimkosoe. Kila nikimkosoa kijakazi huyo huwa anamtetea na tunagombana,” mwanadada aliambia wenzake nao wakamshauri afanye uchunguzi kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wakumbuka mazuri Base Titanium ikijiandaa kufunga...

Ada ya kujipatia paspoti yaongezwa huku Ruto akiwinda pato...

T L