• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:36 PM
Ghulamu mtukutu apiganisha wazazi

Ghulamu mtukutu apiganisha wazazi

Na NICHOLAS CHERUIYOT

MOGOIYWET, Narok

GHULAMU mtukutu kutoka eneo hili aliwagonganisha wazazi wake kwa kutoroka kutoka shule ya upili anakosomea akidai alifukuzwa nyumbani kwa kutolipa karo.

Kulingana na mdaku, wiki moja kabla ya tukio baba ya kijana huyo aliuza ng’ombe na kuelekea shuleni kulipa karo na hakutarajia mwanawe kutumwa nyumbani.

Hata hivyo, juzi barobaro alifika nyumbani na kudai aliambiwa asirudi shuleni hadi karo yote ilipwe.

Moja kwa moja, mume na mke waligombana, mke akilaumu mumewe kwa kufuja hela badala ya kulipa karo huku mumewe naye akijitetea vilivyo.

“Kumbe uliuza ng’ombe na kwenda kutumia pesa hizo vibaya! Nimekuwa nikishuku kuwa una mpango wa kando na sasa nimeanza kuamini. Ona sasa, mtoto amekosa vipindi shuleni,” mke akafoka kwa hamaki.

“Shida yako ni kulipuka kama bomu bila kuchunguza mambo. Labda hesabu za shule hazikufanywa vizuri ama huyu kijana anatuhadaa. Tutulie tuchunguze mambo,” jamaa akateta akihema kwa kasi.

Kijana naye alidakia kujitetea na kutaka apewe pesa yeye mwenyewe apeleke shuleni, jambo ambalo lilmkasirisha baba zaidi.

“Kama hela za ng’ombe hazijulikani zilipotea vipi mikononi mwa baba, basi tuuze ng’ombe mwingine mimi nipeleke hela moja kwa moja hadi shuleni nilipe mwenyewe,” kijana akasema.

Baba ya kijana aliona hakukuwa na haja ya mabishano na akaamua kupiga simu hadi shuleni kujua ukweli wa mambo.

“Aliambiwa shuleni kuwa kijana hadaiwi chochote bali aliamua kutoroka shuleni,” mdaku akaeleza.

Mzee alinguruma kumtaka kijana aandamane naye hadi shuleni huku mkewe akiomba msamaha kwa kumshuku kutokana na udanganyifu wa kijana huyo.

You can share this post!

Watishia kususia uchaguzi mkuu mwaka 2022 kiwanda cha miwa...

KIKOLEZO: Utamu wa chai si rangi!

T L