• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Waumini wafokea pasta dikteta

Waumini wafokea pasta dikteta

Na TOBBIE WEKESA

UGWERI, RUNYENJES

WAUMINI wa kanisa moja lililoko hapa walitishia kumtimua pasta wao wakidai alikuwa dikteta.

Waumini hao walikasirishwa na uamuzi wa pasta huyo kuweka kiwango cha chini cha sadaka ambacho kila muumini alifaa kutoa.

Kulingana na mdokezi, baada ya ibada pasta alitoa tangazo kwa waumini wote.

“Waumini wapendwa ninalo tangazo moja,” pasta alianza kusema.

Waumini walitulia kumsikiliza pasta.

“Nimehudumu na nyinyi miaka mingi. Tumefanya maombi mengi sana tukitaka Mungu atufungulie milango ya ufanisi,” pasta aliwaeleza waumini. Kila wakati hatupigi hatua yoyote. Naona ni kama wengine wenu huwa hamuombi. Kuanzia leo hakuna mtu kuja na sadaka ya shilingi hamsini,” pasta alitangaza.

Inadaiwa waumini walianza kuangaliana huku wakisemezana kwa sauti za chini.

“Huyu mtu leo amevuta bangi ya wapi? Ameona sisi tunapalilia pesa kwetu,” muumini mmoja alisikika akisema.

Duru zinasema pasta alianza kutaja miradi iliyofaa kutekelezwa.

“Tuna miradi mingi sana ya kutekelezwa. Iwapo utakuja na sadaka chini ya kiwango nilichotaja, usilete hapa. Itakuwa bora hata usije kanisani,” pasta aliwaeleza waumini.

Habari zilizotufikia zinasema waumini waliinuka na kuanza kumfokea pasta.

“Sisi tutaleta chochote tutakachopata hata kama shilingi kumi,” muumini alifoka.

Inadaiwa pasta alishindwa kuwadhibiti waumini.

“Kwanza hizi nguo unazobadilisha kila Jumapili tunashuku unatumia sadaka yetu kuzinunua. Tutachunguza,” pasta alifokewa.

Duru zinasema waumini hawakumpa pasta muda kujieleza.

“Wewe mwenyewe huna chochote. Sadaka yenyewe huwa hutoi. Unatupa masharti kama nani,” pasta alizomewa.

Kwa kuhofia usalama wake, pasta alianza kuomba msamaha.

“Wewe ni dikteta. Na ukiendelea hivi hutakaa hapa,” waumini waliapa.

You can share this post!

Marumo Gallants anayochezea Mkenya Ovella Ochieng’...

JAMVI: Kuna hatari ya Raila ‘kujikwaa’ kisiasa kwa...