• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
Wazee wadai ‘kitu kidogo’ kwa mganga

Wazee wadai ‘kitu kidogo’ kwa mganga

Na TOBBIE WEKESA

MSAKASA, Bungoma

KIZAAZAA kilizuka eneo hili baada ya wazee kumlazimisha mganga kuwagawia sehemu ya faida inayotokana na kazi yake au waivuruge.

Kulingana na mdokezi, wazee kadha kijijini walikusanyika na kuelekea kwa mganga.

“Vipi mzee mwenzetu. Umekuwa mganga maarufu. Hela umejizolea nyingi sana. Tumejileta hapa ili utumegee kidogo,” mganga alielezwa.

Duru zinasema mganga aliwaangalia wazee hao kisha akaanza kuwazomea.

“Nimelelewa na nyinyi hapa. Nimezeeka na nyinyi. Mimi sipendi watu wazembe,” mganga aliwakemea wazee.

Inadaiwa wazee hawakutishika na semi za mganga.

Waliapa kutoondoka hadi mganga atimize maombi yao.

“Hapa hatutoki mikono kavu. Hii mali yote umepata kutokana na kazi ya uganga. Hakuna vile utafurahia kula nyama na sisi tunapambana na mboga za matawi,” wazee walifoka.

Duru zinasema mganga alitishia kuwachukulia hatua wazee hao.

“Naona mmeanza kuingilia kazi yangu. Kama mnataka kula nyama kama mimi njooni niwafunze kazi,” mganga aliwaambia wazee wenzake.

Inaarifiwa kuwa wazee walitishia kuvuruga kazi ya mganga.

“Kwa muda mrefu tumekupa amani na utulivu ili ufanye kazi yako vyema. Umetajirika kwa kutapeli watu na tumekuwa tukinyamaza tukijua vituko vyako. Hata sisi tunakuchukulia hatua na tuone nani ataenda hasara,” wazee walitishia.

Habari zilizotufikia zinasema wazee waliapa kuwaonya watu kijijini na nje ya kijiji dhidi ya kuenda kwa mganga.

“Huwa unawadanganya watu kuwa wewe ni daktari wa kutibu magonjwa yote ilhali hukuweza kumtibu mkeo. Wewe ni mkora na tutawatangazia watu,” wazee walitisha.

Mdaku aliarifu kuwa, mganga alipoona kazi yake imo hatarini, aliwarai wazee wawe watulivu.

“Niko tayari kutimiza maombi yenu. Msiniharibie kazi,” mganga aliwarai wazee.

You can share this post!

Wakulima Bondeni walia bei duni za viazi na kupunjwa na...

Mali fiche yafichuka