NA JANET KAVUNGA
SOKOKE, KILIFI
WAZEE katika kijiji kimoja hapa walifanya tambiko kumtakasa mwanadada mmoja baada ya kulaaniwa na nyanya ya mumewe.
Yasemekana mwanadada huyo alimkosea heshima nyanya ya mumewe kwa kumtusi anaye akatamka maneno ya laana kwa hasira.
Maneno hayo yalianza kumwathiri mwanadada huyo akawa anaishi maisha ya masononeko hadi akatubu na kwenda kwa wazee wamsaidie.
“Mwanadada aliandamwa na masaibu chungu nzima hadi akakumbuka maneno ya nyanya ya mumewe alipomkosea. Alitubu na kumuomba amsamehe naye ajuza huyo akakubali,” alisema mdokezi wetu.
Baada ya nyanya kukubali msamaha, wazee waliandaa kafara ambayo mwanadada aligharimika pakubwa. Hata baada ya tambiko walimuonya dhidi ya kuwadharau wazee.