Habari za Kitaifa

Dorice Donya asema angekuwa hana mume angesubiri ‘boyfie’ aliyesomea Maranda

March 8th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

MBUNGE Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Kisii Dorice Donya Aburi mnamo Alhamisi aliibua kicheko Bungeni alipodai angalirudi kuwa kigoli asiye na mume, angalisubiri mpenzi wa kiume ambaye amesomea shule ya kitaifa ya wavulana ya Maranda High.

Bi Aburi alisema hayo baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kuwajulisha wabunge kuhusu uwepo wa kundi la wanafunzi kutoka shule hiyo ya upili iliyoko Kaunti ya Siaya miongoni mwa shule nyingine.

“Mheshimiwa Spika, shule hii ina sifa ya kufanya vizuri katika mtihani wa kitaifa kiasi kwamba ingalikuwa ni enzi zile za kuandikiana barua za mapenzi ningalitamani kuwa na rafiki kutoka shule hii,” akasema huku wabunge wenzake wakiangua kicheko.

Lakini Bi Aburi alikuwa mwepesi wa kufafanua kuwa Shule ya Upili ya Kitaifa ya Kisii School katika kaunti yake ya Kisii, pia hufanya vizuri katika mtihani wa kitaifa.

Alisema hayo baada ya Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa Maranda High kupewa fursa na Spika Wetang’ula kuwakaribisha wanafunzi hao.

Bw Amollo, alisifia shule hiyo akisema imefaulu kufinyanga watu mashuhuri nchini akiwemo yeye na kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga, miongoni mwa wengine.

Naye Mbunge wa Alego Usonga Samuel Atandi alisema wanafunzi wengi werevu kutoka eneobunge lake husomea katika shule hiyo ya upili chini ya ufadhili wa Hazina ya Ustawi wa eneobunge hilo (NG-CDF).