Michezo

Dortmund kukamilisha usajili wa tineja wa Birmingham City wiki hii

June 23rd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BORUSSIA Dortmund wanatarajia kukamilisha usajili wa kiungo Jude Bellingham kutoka Birmingham City kufikia Juni 27, 2020.

Agosti 2019 Bellingham alivunja rekodi ya mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Trevor Francis kwa kuwa mchezaji wa umri wa chini zaidi kuwahi kuchezea Birmingham baada ya kupangwa katika kikosi cha kwanza akiwa na umri wa miaka 16 na siku 38.

Bellingham alifunga bao dhidi ya Stoke City katika mechi yake ya kwanza kambini mwa Birmingham.

Tangu wakati huo, amewajibishwa mara 36.

Manchester United ndicho kikosi cha kwanza kuanza kuwania maarifa ya Bellingham ambaye kwa sasa ni tegemeo kubwa kambini mwa timu ya Uingereza ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 17.

Ni matarajio ya Dortmund kwamba watatumia mfano wa Jadon Sancho kumshawishi Bellingham kujiunga nao rasmi kufikia mwisho wa msimu huu.

Nyota ya Sancho ambaye kwa sasa anawaniwa pakubwa na Man-United na Real Madrid, ilianza kung’aa baada ya kubanduka Ujerumani na kutua Manchester City akiwa na umri wa miaka 17 pekee.