Michezo

DORTMUND MOTO: Schalke 04 yapata kichapo 'saizi' ya jina lake

May 16th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BORUSSIA Dortmund imepata ushindi wake wa kwanza tangu mwaka 2015 katika uwanja wake wa nyumbani wa Signal Iduna Park dhidi ya Schalke baada ya kutitiga wageni hao 4-0, huku Ligi Kuu ya Ujerumani ikirejea kwa kishindo baada ya kusimama kwa miezi miwili kwa sababu ya janga la virusi hatari vya corona.

Mabingwa hao wa mataji matano ya Bundesliga, ambao walishinda ligi hii mara ya mwisho msimu 2011-2012, waliingia mchuano dhidi ya Schalke na motisha kubwa ya kushinda Eintracht Frankfurt 4-0, Werder Bremen 2-0, Freiburg 1-0 na Borussia Monchengladbach 2-1 ligini katika mechi nne zilizopita.

Hata hivyo, walikuwa wamepiga Schalke mara moja tu katika mechi nane zilizopita, na ilikuwa ugenini walipolaza timu hiyo 2-1 mwezi Desemba 2018.

Ushindi wa mwisho wa Dortmund uwanjani Iduna dhidi ya Schalke ulikuwa 3-2 Novemba 8, 2015.

Dortmund ilimaliza nuksi hizo kwa kupitia mabao ya mshambuliaji matata Erling Haaland dakika ya 29, beki Mreno Raphael Guerreiro dakika ya 45 na 63 na kiungo Mbelgiji Thorgan Hazard.

Hazard, ambaye ni nduguye nyota wa zamani wa Chelsea Eden Hazard, alimegea Haaland krosi safi kutoka pembeni kulia kufungua ukurasa wa magoli.

Mjerumani Julian Brandt alipasia Guerreiro, ambaye aliadhibu kipa Markus Schubert aliyekuwa ameanzisha mpira vibaya kwa kupigia mpinzani baada ya Haaland kumwekea presha ndani ya kisanduku.

Hazard aliongeza bao la tatu baada ya kupokea krosi kutoka kwa Brandt pembeni kushoto na kusukumia kipa kiki zito hadi wavuni.

Brandt alikuwa amepokea mpira kutoka kwa Haaland, ambaye alikuwa amechezewa visivyo, lakini refa akaacha mpira uendelee baada ya Brandt kuufikia.

Guerreiro alihitimisha kwa kufunga bao safi kupitia mguu wake hatari wa kushoto kutoka pembeni kulia baada ya kuanzisha shambulio na kisha kukamilisha pasi kutoka kwa Haaland.

Dortmund sasa ana alama 54, moja nyuma ya mabingwa watetezi Bayern Munich, ambao watavaana na Union Berlin hapo Jumapili.

Katika mechi zingine ambazo zimesakatwa leo Jumamosi, Augsburg imepoteza nyumbani 2-1 dhidi ya Wolsfburg, Dusseldorf na Paderborn zikaumiza nyasi bure katika sare ya 0-0 nayo Hoffenheim ikalizwa 3-0 na Hertha Berlin.

Mechi kati ya RB Leipzig na Freiburg imetamatika 1-1.