Dortmund wakataa ofa ya Sh9.4 bilioni ambazo Man-United wako tayari kutoa kwa ajili ya Sancho

Dortmund wakataa ofa ya Sh9.4 bilioni ambazo Man-United wako tayari kutoa kwa ajili ya Sancho

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

OFA ya Sh9.4 bilioni ambayo imetolewa na Manchester United kwa ajili ya kumsajili fowadi matata raia wa Uingereza, Jadon Sancho imekataliwa na Borussia Dortmund ambao ni waajiri wa sogora huyo nchini Ujerumani.

Badala yake, Dortmund wanataka kima cha Sh10.9 bilioni kwa ajili ya huduma za mvamizi huyo mwenye umri wa miaka 21 kisha salio la Sh595 milioni lilipwe chini ya kipindi cha mwaka miaka minne baadaye.Kati ya masupastaa wao wengine, wakiwemo Erling Braut Haaland na Jude Bellingham, Dortmund wako radhi kumuuza Sancho pekee muhula huu.

Awali, Dortmund waliwataka Manchester United kuweka mezani kima cha Sh11.4 bilioni ili waanze kujivunia huduma za Sancho.

Iwapo Man-United wangeshawishika kufanya hivyo, basi wangekuwa wameokoa Sh3.7 bilioni kutoka kwa Sh15.1 bilioni zilizokuwa zikidaiwa na Dortmund kwa ajili ya uhamisho wa sogora huyo hadi Old Trafford mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Kufaulu kwa mpango huo wa kusajiliwa kwa Sancho kutamfanya awe mchezaji wa pili ghali zaidi kuwahi kutua Old Trafford baada ya kiungo Paul Pogba kusajiliwa na Man-United kwa kima cha Sh12.4 bilioni kutoka Juventus ya Italia mnamo 2016.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer ambaye ni raia wa Norway, Man-United waliweka mezani kima cha Sh11.2 bilioni ili kumshawishi beki na nahodha Harry Maguire kuagana na Leicester City ugani King Power miaka miwili iliyopita.

Huku Dortmund wakitaka fedha zote za mauzo ya Sancho kutolewa pamoja, Man-United wangependelea kukamilisha malipo hayo kwa awamu mbili.

Dortmund wako radhi kumwachilia Sancho aondoke ugani Old Trafford ili wasalie na fowadi raia wa Norway, Halaand anayemezewa pia na Manchester City ambao wanatafuta mfumaji mrithi wa Sergio Aguero aliyeyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona.

Man-City na Man-United wanamhemea pia fowadi na nahodha wa Tottenham Hotspur, Harry Kane.Licha ya kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2021-22, Dortmund wana ulazima wa kuagana na baadhi ya wanasoka wao wa haiba kubwa muhula huu ili kupunguza gharama ya matumizi baada ya janga la corona kulemaza hazina yao.

Ili kukatiza tama ya Man-City kumfukuzia Haaland, Dortmund wamefichua kwamba bei mpya ya fowadi huyo wa zamani wa RB Salzburg ni Sh19.6 bilioni. Man-City waliokuwa waajiri wa zamani wa Sancho watatia kapuni bonasi ya Sh1.5 bilioni iwapo kiungo huyo mvamizi atatua Man-United.

Sancho alianza kusakata soka ya kulipwa ugani Etihad na alikataa ofa mpya ya mshahara wa Sh4.2 milioni kwa wiki na kuyoyomea Ujerumani akiwa na umri wa miaka 17. Hofu yake ilikuwa ni kukosa uhakika wa kuunga kikosi cha kwanza cha Man-City chini ya kocha Pep Guardiola aliyekuwa ametokea Bayern Munich wakati huo.

Kufikia sasa, Sancho amfungia Dortmund mabao 50 kutokana na jumla ya mechi 137. Anajivunia kufungia timu ya taifa ya Uingereza jumla ya mabao matatu kutokana na mechi 18.

Nyota huyo aliyezaliwa katika eneo la Camberwell, Kusini mwa jiji la London, alijiunga na akademia ya Watford akiwa na umri wa miaka saba kabla ya Man-City kumsajili kwa Sh9.2 milioni pekee akiwa na umri wa miaka 14. Uhamisho wake hadi Dortmund ulishuhudia Watford wakipokezwa na Man-City kima cha Sh70 milioni zaidi.

  • Tags

You can share this post!

Wijnaldum aondoka Liverpool na kuingia PSG kwa mkataba wa...

Covid-19: Fainali za Copa America nchini Brazil kuendelea...