Michezo

Dortmund wamsajili beki matata Thomas Meunier kutoka PSG

June 25th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BORUSSIA Dortmund wamemsajili beki matata mzawa wa Ubelgiji, Thomas Meunier kwa mkataba wa miaka minne kutoka Paris Saint-Germain (PSG).

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 ataingia rasmi kambini mwa Dortmund nchini Ujerumani baada ya kandarasi yake na PSG kutamatika rasmi mnamo Juni 30, 2020.

“Dortmund hucheza soka ambayo nimekuwa nikitamani sana kusakata: inavutia na ina uhalisia mwingi,” Meunier akasema.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa spoti kambini mwa Dortmund, Michael Zorc alisema Meunier ni mchezaji ambaye uwezo wake umejidhihirisha katika soka ya kiwango cha juu na hatatizika kivyovyote kuoanisha mtindo wake wa kucheza na ule wa wenzake kikosini.

Meunier ambaye atatua Dortmund bila ada yoyote, alijiunga na PSG mnamo 2016 baada ya kuagana na Club Bruges ya Ubelgiji. Tangu wakati huo, anajivunia kushindia PSG mataji matatu ya Ligue 1 na ubingwa wa French Cup mara mbili.

Kutua kwake Dortmund ambao wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kunamuunganisha na wanasoka wenzake wazawa wa Ubelgiji – Thorgan Hazard na Axel Witsel.