Michezo

Dortmund washinda mchuano wa kwanza chini ya kocha mshikilizi Terzic

December 16th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MARCO Reus alifunga bao la dakika ya 78 na kusaidia Borussia Dortmund kupepeta Werder Bremen 2-1 katika mechi ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

Ushindi huo ulikuwa wa kwanza kwa Dortmund kusajili chini ya kocha mshikilizi Edin Terzic tangu mkufunzi Lucien Favre atimuliwe na kikosi hicho baada ya kupokezwa kichapo cha 5-1 kutoka kwa Stuttgart.

Reus alifunga bao katika jaribio la pili baada ya penalti aliyoipiga awali kupanguliwa na kipa wa Bremen.

Raphael Guerreiro aliwafungulia Dortmund ukurasa wa mabao kunako dakika ya 12 kabla ya Kevin Mohwald kusawazisha katika dakika ya 28.

Mechi hiyo ilisimamiwa na Terzic akisaidiwa kazi na Sebastian Geppert na Otto Addo ambao ni wakufunzi wa vikosi chipukizi kambini mwa Dortmund. Terzic alipokezwa mikoba ya Dortmund ashikilie hadi mwishoni mwa msimu huu wa 2020-21 baada ya kutimuliwa na Favre.

Kutokuwepo kwa fowadi matata Erling Braut Haaland kulimweka Terzic katika ulazima wa kumpanga chipukizi Youssoufa Moukoko katika kikosi chake cha kwanza.

Ingawa hakuridhisha sasa, chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 16 alimtatiza kipa Jiri Pavlenka mara mbili mwishoni mwa kipindi cha pili. Ushindi wa Dortmund ulikomesha rekodi mbovu iliyoshuhudia kikosi hicho kikipiga jumla ya mechi tatu za Bundesliga bila ushindi.

Alama tatu zilizotiwa na Dortmund kapuni ziliwapaisha ligini hadi nafasi ya nne kwa alama 22, tatu nyuma ya viongozi Bayer Leverkusen.