Michezo

Dortmund wasonga mbele katika UEFA licha ya kukosa Haaland katika mechi dhidi ya Lazio

December 3rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LICHA ya kuzikosa huduma za fowadi tegemeo Erling Braut Haaland, Borussia Dortmund walifuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kulazimishia Lazio ya Italia sare ya 1-1 mnamo Disemba 2, 2020 uwanjani Signal Iduna Park, Ujerumani.

Haaland ambaye kwa pamoja na Alvaro Morata wa Juventus wanaongoza orodha ya wafungaji bora wa UEFA kwa mabao sita kila mmoja hadi kufikia sasa, alikosa kuwa sehemu ya kikosi kilichotegemewa na Dortmund dhidi ya Lazio kwa sababu ya jeraha la paja.

Kukosekana kwake kulihisika pakubwa katika safu ya mbele ya Dortmund ambao walifungiwa bao na Raphael Guerreiro katika dakika ya 44.

Penalti ya mshambuliaji Ciro Immobile katika kipindi cha pili iliwapa Lazio sare ambayo kwa sasa inawaweka katika ulazima wa kujizolea angalau alama moja katika mchuano ujao dhidi ya Club Brugge ya Ubelgiji ili kufuzu kwa hatua ya mwondoano. Club Brugge waliwapokeza Zenit St Petersburg kichapo cha 3-0 katika mchuano mwingine wa Kundi F uliosakatwa Disemba 2, 2020.

Dortmund kwa sasa wanadhibiti kilele cha Kundi F kwa alama 10, moja zaidi kuliko nambari mbili Lazio. Club Brugge wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama saba, sita zaidi kuliko Zenit ya Urusi.