Dosari za uchaguzi zatajwa kuwa tisho

Dosari za uchaguzi zatajwa kuwa tisho

NA WINNIE ONYANDO

TUME ya Kitaifa ya Haki za Binadamu (KNCHR) imegundua dosari nyingi kwenye matayarisho cha Uchaguzi Mkuu wa wiki ijayo, mengi yakihusiana na ukiukaji wa haki.

Kutokana na taasisi husika kutochukua hatua za mapema, sasa KNCHR inahofia kwamba huenda kukazuka vurugu baada ya Agosti 9 hasa katika ngome za wawaniaji wakuu wa urais.

Hapo jana Jumatano, serikali ya Marekani ilitoa tahadhari ya kuwataka raia wake wasizuru jiji la Kisumu ikisema iko na taarifa ya uwezekano wa kutokea machafuko.

Jana Jumatano wakati wa kikao na wanahabari katika hoteli ya The Stanley, Nairobi, mwenyekiti wa KNCHR, Bi Roseline Odede alitoa wito kwa Wizara ya Usalama wa Ndani kuwa macho na kuwatuma maafisa zaidi katika ngome za wawaniaji wakuu wawili, William Ruto na Raila Odinga ili kudhibiti machafuko ya baada ya uchaguzi endapo yatazuka.

Tume hiyo ilisema kuwa kati ya wawaniaji wanne wa kiti cha urais, mmoja tu ndiye aliyetia saini mkataba wa amani.

“Ni David Mwaure pekee aliyeweka sahihi mkataba wa amani baada ya kuidhinishwa kuwania kiti hicho. Kiongozi wa ODM Raila Odinga, Naibu wa Rais William Ruto na Profesa George Wajackoyah kufikia sasa hawajajitokeza kutia saini mkataba wa kudumisha amani na kulinda haki za binadamu,” akasema Bi Odede.

KNCHR pia imetoa wito kwa serikali kupiga darubini mitandao ya kijamii ya Tik Tok, Facebook na WhatsApp kwa kuwa inatumiwa kueneza propaganda na uoga uchaguzi ukikaribia.

Kuhusu suala la usalama, tume hiyo ilisema kuna wasisawi ikiwa wakazi wanaotoka katika maeneo yenye historia ya ghasia watajitokeza kikamilifu kupiga kura. Baadhi ya maeneo hayo ni Baringo, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi na Marsabit.

Serikali inaendeleza kanuni za kafyu katika maeneo hayo, na sasa tume hiyo inasema huenda wakazi wasipige kura wasipohakikishiwa usalama wao.

Ripoti ya awali ilionyesha kuwa serikali ilipanga kuhamisha baadhi ya vituo vya kupigia kura katika kaunti ndogo za Baringo Kusini na Baringo Kaskazini kutokana na ukosefu wa usalama.

Taarifa hiyo pia inaonyesha kuwa migogoro ndani ya vyama mbalimbali imesababisha visa 50 vya mashambulizi na vurugu huku visa 146 vya watoto kutumiwa kwenye kampeni vikishuhudiwa.

Tume hiyo imeonya pia kuhusu matamshi ya wanasiasa ya madai ambayo hayawezi kuthibitishwa, ikisema ni sawa na uchochezi.

Kufikia sasa, tume hiyo imerekodi visa 44 vya matumizi mabaya ya rasilimali za umma katika ngazi ya kaunti na serikali ya kitaifa hasa wakati wa kampeni.

  • Tags

You can share this post!

Pogba kusakata Kombe la Dunia

Kura: Machifu hawapigii debe Azimio – Kibicho

T L