DOUGLAS MUTUA: Jumatatu si sikukuu rasmi

DOUGLAS MUTUA: Jumatatu si sikukuu rasmi

NA DOUGLAS MUTUA

IKIWA una akili timamu, unajua Jumatatu hii si sikukuu. Vilevile, ikiwa una akili timamu, unajua maandamano yanayopangwa kufanyika siku hiyo kwenda Ikulu si ya amani.

Tangazo la kiongozi wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga kwamba siku hiyo itakuwa sikukuu si mzaha, ni jambo la kutafakariwa.

Kisa na maana Bw Odinga ana wafuasi wengi tu wasiojali matokeo ya tangazo hilo katika maisha yao; ilimradi ametamka neno tu, watatii na kufanya atakavyo.
Hii ina maana kwamba wapo wasiotumia akili watasusia kazi, labda wafutwe kisha wafutwe, nazo familia zao ziendelee kuteseka.

Wajuaji watakwambia si neno, watu hao tayari wanalala njaa, kazi zao hazikidhi mahitaji yao, hivyo wakifutwa hakutakuwa na mabadiliko yoyote.

Si kweli; asiye na kazi, hata ikiwa mbaya kiasi gani, si sawa na aliye nayo. Kazi mbi, si mchezo mzuri, Mswahili anakwambia, na huo wa maandamano ni mchezo mzuri ila usio na tija.

Nimesema hayo si maandamano ya amani kwa kuwa chanzo chake ni malalamiko ya Bw Odinga kwamba aliibiwa kura wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita mwezi Agosti 9, 2022.

Unapoandaa maandamano dhidi ya mtu unayedai aliiba kura zako, eti umfuate Ikulu, kila mtu anayetumia akili anajua hilo ni jaribio la kupindua serikali!

Na usitarajie serikali itakuandalia chai huko ikulu, mnywe kisha ikuage na kuondoka, eti uwe mwenyeji mpya. Nguvu za dola zitatumika kulinda mamlaka ya rais kwa vyovyote vile.

Tatizo kwamba watakaoumizwa ni hao niliotilia shaka utimamu wa akili zao, ila maji yakizidi unga, aliyeandaa maandamano ataondolewa ghafla kwa magari ya kifahari huku akilindwa kama mfalme.

Labda Bw Odinga, katika kuhimiza wafuasi wake waandamane hadi Ikulu, amechochewa na tukio kama hilo lililofanyika nchini Sri Lanka mwaka 2022.

Nia ilikuwa kumwondoa mamlakani Rais Gotabaya Rajapaksa kutokana na kile waandamanaji walichokiita utawala mbaya uliozorotesha uchumi wa nchi kupita kiasi.
Waandamanaji walifika ikulu kwa maelfu, wakafurika humo na kuharibu mali, wengine wakaonekana wakilala kwenye kitanda cha rais na kujiburudisha kwa vinyaji na vyakula vyake.
Kando na kulalamika kuhusu kura zake, Bw Odinga anateta kwamba matatizo ya kiuchumi yanayoikumba Kenya hayavumiliki, dai ambalo wengi watakubaliana nalo.

Hatari ndiyo hii: Nina hakika Rais William Ruto, kama Bw Odinga, alitazama video hiyo ya raia wakivamia ikulu ya rais nchini Sri Lanka na hataketi kitako na kusubiri kufurushwa Ikulu.

Kama kiongozi wa nchi, Bw Ruto ana habari kwamba maandamano ya aina hiyo yamepangiwa kufanyika siku hiyo nchini Afrika Kusini, Nigeria na Tunisia.

Kama mwanasiasa aliyeshuhudia serikali nyingi zikitikiswa na harakati za kudai siasa za vyama vingi mapema miaka ya tisini, anazielewa vyema athari za matukio hayo.

Kama amiri jeshi mkuu, haikosi atatumia mamlaka yake kuzima maandamano hayo. Hii ina maana kwamba vurugu itazuka.
Wapo watakaovunjwa mbavu; wapo watakaouawa. Wanamapinduzi watakwambia haijalishi kwamba madai ya Bw Odinga kwamba kura zake ziliibwa yalishughulikiwa kikamilifu na Mahakama ya Upeo, lazima Ruto aondoke! Hapo ndipo unapohitajika kutumia akili vizuri, si kama kofia. Ukifaulu kufanya hivyo, swali la kimsingi linaibuka akilini mwako: Nina haki ya kupindua serikali halali?
Uhalali wa serikali ya sasa, hasa kwa kuwa ulishathibitishwa na idara ya mahakama, unaweza kusababisha Bw Odinga apoteze uungwaji mkono nchini na kimataifa kwa kiasi kikubwa. Tayari umejionea marafiki zake wa humu nchini wanavyomkimbia.
Akitaka heshima zake zidumu, Bw Odinga ajitwike jukumu la kuimarisha upinzani rasmi, si kupindua serikali halali. Ameisha nguvu za mapinduzi! Tahadhari uunusuru uhai wako.

mutua_muema@yahoo.com

  • Tags

You can share this post!

Kenya U13 yaelekea Uingereza kwa raga za kimataifa za...

Angika daluga za ulingo wa kisiasa, Kidero amwambia Raila

T L