DOUGLAS MUTUA: Kenya, Afrika zitafaidikaje kwa utawala wa biden?

DOUGLAS MUTUA: Kenya, Afrika zitafaidikaje kwa utawala wa biden?

Na DOUGLAS MUTUA

SERIKALI mpya ya Marekani inatarajiwa kuwa na athari kubwa nchini Kenya na barani Afrika kwa jumla ikilinganishwa na iliyoitangulia.

Rais Joe Biden, aliye na sifa za uzoefu mwingi tu katika mashauri ya kimataifa, anatarajiwa kuwa na sera tofauti kabisa na za mtangulizi wake, Bw Donald Trump.

Tofauti na Trump, Biden anatarajiwa kuwaheshimu Waafrika zaidi na kutafuta urafiki nao. Trump hakujali wala kubali Waafrika tungalimchukuliaje, alitenda aliyoyataka.

Kwa mfano, Biden anatarajiwa kuheshimu jumuiya na mashirika ya mataifa ya Afrika na hivyo basi kuyawezesha kujiimarisha badala ya kuyasambaratisha.

Hiyo ndiyo mbinu anayotarajiwa kutumia ili kukabiliana na ushawishi mkubwa wa Uchina barani Afrika ambao unatishia ule wa Marekani uliodumu miongo mingi.

Kwa mfano, zipo sera nyingi tu ambazo zinatarajiwa kuifaa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa jumla badala ya kuhusiana moja kwa moja na mataifa binafsi ya kanda hii.

Lisilojulikana na wengi ni kwamba uamuzi wa Trump kujadiliana moja kwa moja na Rais Uhuru Kenyatta Kenya kuhusu biashara na uhusiano wa Marekani na Kenya ulizua taharuki Afrika Mashariki.

Kisa na maana ni kwamba Jumuiya ya EAC ina sera za kibiashara ambazo mataifa wanachama huzingatia yanapohusiana na yasiyo wanachama kwa manufaa ya pamoja.

Hivyo basi, Serikali ya Trump ilipoanzisha mashauri na Kenya kuhusu ushirika wa kibiashara kati ya mataifa yote mawili bila kupitia jumuiya ya EAC, hilo halikuyakaa vizuri mataifa mengineyo.

Kenya ilichukuliwa kama msaliti wa majirani na ndiyo maana mara nyingi Tanzania ililalamika kwamba tunapendelewa na Marekani.

Uganda nayo, ingawa haikutupiga vijembe moja kwa moja, ilianza kuhusiana na Tanzania kwa karibu zaidi, ishara kwamba Kenya haikuaminika na ilitengwa kimya-kimya.

Utawala mpya wa Biden ukianzisha mashauri ya aina hiyo na Jumuiya ya EAC badala ya nchi binafsi, uhusiano kati ya mataifa wanachama utaimarika kwa kiasi kikubwa.

Na hiyo ni hatua nzuri kwa sababu yapo manufaa mengi ambayo Kenya itapata kutoka kwa majirani kama Tanzania na Uganda uhusiano huo ukiimarika.

Kwa mfano, Tanzania na Uganda zinazalisha umeme kwa kiasi kikubwa sana hivi kwamba unatosha kutumika nchini na masalio kuuzwa nje.

Kenya bado hatujafikia kiwango hicho, hivyo basi tutakuwa wateja wa kwanza kunufaika na maendeleo hayo ya majirani zetu almradi tupunguze kiburi.

Hata hivyo, yapo mambo ambayo kwayo Marekani itahusiana na Kenya moja kwa moja. Mathalan, Kenya na Marekani zinakabiliwa na changamoto ya kipekee: ugaidi.

Ili kuikabili hatari hiyo kikamilifu, nchi hizo mbili zitahusiana moja kwa moja na hivyo basi madola yatamiminika kwa wingi tu kutoka Washington D.C.

Vilevile, kampuni za Marekani ambazo zimekuwa zikifanya shughuli nchini Kenya zinatarajiwa kuendelea kuwapo wakati wa utawala wa Bw Biden.

Kwa mfano, kampuni ya Delmonte inayokuza mananasi na vyakula mbalimbali nchini Kenya itaendelea na shughuli zake bila bughudha hata kidogo.

Makubaliano kati ya Kenya na Marekani ya kuandika upya mkataba wa kuipangisha Delmonte ardhi yaliyofanyika mwaka jana hayataathiriwa na utawala mpya.

Ahadi ya kampuni hiyo kujenga hospitali ya rufaa na mafunzo kwenye Kaunti ya Murang’a itakayogharimu jumla ya Sh3 bilioni itatekelezwa.

Miradi mingine iliyolenga afya na elimu, ambayo ama ilikatizwa au ikapunguziwa fedha na utawala wa Trump inatarajiwa kupata nguvu mpya.

Kwa jumla, ili kuhusiana vizuri na Afrika, utawala wa Biden unatarajiwa kuendeleza sera za Rais wa 44 wa Marekani, Barrack Obama, aliye na asili ya Kenya.

Hata hivyo, yote hayo si kwa ajili ya kuifanyia hisani Afrika bali kwa manufaa ya Marekani, hivyo ni jukumu la Afrika kutumia fursa hiyo kujinufaisha.

mutua_muema@yahoo.com

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tusimhukumu Trump, tujifunze kutoka kwa...

MWANAMUME KAMILI: Kila nyumba huwaka moto, muhimu kujenga...