DOUGLAS MUTUA: Kumbe wanasiasa Kenya watoshana nguvu, ujanja!

DOUGLAS MUTUA: Kumbe wanasiasa Kenya watoshana nguvu, ujanja!

NA DOUGLAS MUTUA

SI uchaguzi huu umewafunza Wakenya mambo mengi?

Funzo kuu kati ya yote ni umuhimu wa kuwa na subira. Kile kiherehere cha tangu hapo cha kudai matokeo usiku wa uchaguzi au siku inayofuata kimepata tiba eti.

Kisa na maana? Hamna mitambo ya siri inayohodhi matokeo kama ilivyokuwa katika Uchaguzi Mkuu 2017.

Mara hii vyama, wawaniaji wa chaguzi mbalimbali na wanahabari wameruhusiwa kuingia yanamohifadhiwa matokeo, kila mmoja akajua changamoto za kuyatangaza upesi ambazo zimekuwa zikiwakumba waandalizi.

Mwisho wa kiherehere chetu ni pale ambapo mtu binafsi anajaribu kufanya hesabu rahisi za kuunga idadi za kura ili kumjua mshindi ila anakwama kwa kuchoka au kukanganyikiwa.

Hivyo ndivyo ambavyo kelele za kuibiwa, kucheleweshewa matokeo na madai mengine ya wajanja waitwao wanasiasa zilivyoshughulikiwa.

Hata hivyo, kwa sababu Wakenya ni wale wale, madai ya karatasi za kupigia kura kuibwa yametolewa na upande mmoja, wa pili nao ukasema ni maigizo tu, wananchi wa kawaida tukabaki kujiuliza ni nani kati ya wajanja hao ambaye ni msema kweli.

Hiyo ni hali nzuri sana. Imetuepushia visa vya watu kulana maini, kuharibu mali na kuhasimiana kipumbavu bila kuwa na hakika ya kinachoendelea.

Sasa nimejua kila maradhi yana tiba, waganga tu ndio ambao hawajaigundua.

Somo la pili nililopata kutoka uchaguzi huu ni kwamba, binadamu haishi unafiki. Yaani wewe na jirani yako mmefanya kampeni pamoja.

Mmeshiriki mikutano ya siasa pamoja huku mkiunga mkono upande mmoja kwa zaidi ya miaka minne.

Ajabu, matokeo yanapoashiria kwamba mpinzani wenu anakaribia kushinda, ghafla mwenzako anapiga ukemi wa ushangilizi!

Kumbe muda huu wote uliyemdhani mwenzako ni jasusi wa upande pinzani!

Unathibitisha hilo pale matokeo hayo yanayopeperushwa mubashara na runinga yanapobadilika ghafla na kuashiria sasa unayemuunga mkono anaongoza. Uliyemdhani mwenzako wa miaka mingi uliyetambua ghafla kwamba ni jasusi anafyata kabisa na kuondoka mtandaoni asishuhudie upande wake ukilimwa.

Yaani haamini kazi yake ya miaka yote hiyo imekuwa bure kabisa!

Somo la tatu ambalo nimepata ni kwamba, Kenya hii hakuna mwanasiasa hodari sana kushinda wote, wanatoshana nguvu.

Ama kweli ujanja, mikakati na wingi wa mafedha havina ushawishi mkubwa mno, nchi imegawanyika mara mbili – nusu kwa nusu.

mutua_muema@yahoo.com

  • Tags

You can share this post!

Tufani ya UDA yamsomba mkuu wa kampeni za Raila

Afisa wa IEBC aliyepoteza matokeo ndani

T L