DOUGLAS MUTUA: Mnyanyaso wa ngono kazini ukabiliwe

DOUGLAS MUTUA: Mnyanyaso wa ngono kazini ukabiliwe

Na DOUGLAS MUTUA

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO) limeapa kuwaadhibu maafisa wake waliowanyanyasa wanawake kimapenzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Manyanyaso hayo ya ngono yalifanyika wakati ambapo maafisa hao walikuwa katika shughuli ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola kati ya mwaka 2018 na 2020.

Yaani watu walioaminiwa kuiepushia dunia nzima maafa walikuwa na muda wa kufanya mambo mengine kando na dharura iliyokuwepo! Uhayawani, au maradhi ya akili hayo?

Ripoti ya wachunguzi huru inaonyesha maafisa wa kigeni walishirikiana na wenzao wenyeji kuajiri na kufuta watu kazi kutegemea huduma ya ngono.

Mkuu wa shirika hilo, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus, amekuja juu baada ya kupokea ripoti hiyo na kuapa kuwachukulia hatua kali wote waliohusika. Ameomba na msamaha.

Wapo waliofutwa kazi kwa kukataa kulala na wakuu wao kazini, na vilevile wapo walioajiriwa kwa kukubali kutoa huduma hiyo kwa wasimamizi wa mradi huo wa WHO.

Labda umezoea kusikia mambo kama haya hivi kwamba huoni kama ni hoja, ati anayetoa huduma kataka mwenyewe, lakini ni makosa makubwa sana katika dunia ya wastaarabu.

Manyanyaso ya ngono na ubakaji yapo kwenye kiwango sawa kwa kuwa katika hali zote mbili hamna hiari bali shinikizo na matumizi ya nguvu ambayo humdhalilisha mhanga.

Unapoanza kuyachukulia kuwa jambo la kawaida, basi jua ama umepotoka kupindukia au una tatizo fulani la akili linalopaswa kuchunguzwa.

Inaudhi sana unapotambua kuwa katika jamii yetu, hasa Afrika, ngono imetokea kuwa kigezo kikuu cha kuwapa watu kazi au kuwashusha madaraka kiasi cha kuzoeleka.

Hatuwezi kuendelea kuishi kama wanyama katika enzi hii ambapo dunia imeunganishwa na teknolojia na kuwa kijiji kimoja. Ni sharti tujiheshimu kwanza ili tuheshimiwe.

Ni maudhi kwa kuwa maafisa hao waliotoka mataifa ya kigeni, hasa Uropa na Marekani, hawawezi kuthubutu kufanya mambo hayo kwao kwani watafungwa jela.

Lakini walijasiria kuyafanya nchini DRC kwa kuwa walichukulia huko ni porini, mbali sana na ustaarabu waliozoea, hivyo watakwepa sheria.

Na walijua ni rahisi kufanya mambo hayo Afrika kwa maana imekuwa desturi yetu kuwadharau wanawake, si ajabu madume wenyeji walikuwa radhi kushirikiana nao.

Hili si jambo geni kwetu Kenya; wawekezaji kutoka Asia na Uropa wanajulikana kwa utundu wa kutumia ngono ili kuwatenga na kuwatawala wafanyakazi wao Wakenya.

Ngono imetumika kwa njia hiyo hata katika ofisi kubwa-kubwa. Watu waliofuzu kikamilifu wamenyimwa kazi kwa kuwa wanaowania fursa nao wamekubali kulazwa!

Hii ni kashfa ambayo inaendelea kuanzia viwandani, hasa vinavyozalisha bidhaa za kuuzwa nje, hadi ofisi kubwa zaidi nchini.

Waulize wanaume watakwambia mara nyingi tu wamenyimwa fursa na wanaume wenzao, wanawake wakapendelewa. Hawatangazi hadharani wasikose kazi kwingineko.

Ajabu akidi ni kwamba kwa jumla wanaume wengi waliowahi kuathirika hivyo huchukulia kuwa wanawake wanapenda sana kutumika hivyo. Si kweli!

Kwanza tuelewane hapa: Kuna wanawake wengi mno ambao wana heshima zao, wanapata kazi kwa sababu wamehitimu na hawapendi masihara hata kidogo.

Lakini pia kuna wengi wanaolazimika kukubali masharti hayo magumu na maovu ya kazi, ambayo kwa hakika si rasmi, bila kujua wananyanyaswa.

Wanadhani wanapendwa. Na wanataka kutoa ‘ahsante’ yao kwa kupewa fursa ya kupata unga.

Ukweli huwapambazukia baada ya kuajiriwa kwa njia hiyo, kisha baada ya kitambo kidogo wengine wanaotamanisha zaidi wanaajiriwa hivyo-hivyo na kuwahatarishia kazi.

Swali kuu: Mbona jamii imewaruhusu wanaume waovu kuendelea kuwanyanyasa wanawake na wanaume wenzao namna hii?

Ama unadhani mwanamume anayenyimwa kazi kwa kuwa mwanamke amependelewa hakunyanyaswa?

Vita dhidi ya manyanyaso ya ngono vinapaswa kuwa vya kila mtu, tena jinsia zote mbili, kwa kuwa uovu huo unaathiri jamii nzima.

mutua_muema@yahoo.com

You can share this post!

Ni makosa UN kuzitenga nchi zilizo na misukosuko

Itumbi alia korti kumzuia kuhusisha mlalamishi na UDA