DOUGLAS MUTUA: Siri ya kuandaa uchaguzi huru ni kuheshimu sheria

DOUGLAS MUTUA: Siri ya kuandaa uchaguzi huru ni kuheshimu sheria

NA DOUGLAS MUTUA

MJADALA unaoendelea kuhusu ufaafu wa teknolojia – au ukosefu wake – kutumika katika Uchaguzi Mkuu ujao unapendeza.

Muungano wa Kenya Kwanza unasema teknolojia pekee itumike kuwatambua watu waliosajiliwa kupiga kura, nao wa Azimio unasema heri sajili iliyochapishwa pia itumike kwani teknolojia inaweza kukwama.

Umenikumbusha propaganda ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto walipokuwa washirika wa kisiasa wakijidai kuwa viongozi wa kidijitali ambao wangeleta mabadiliko nchini.

Walimsawiri kinara wa uliokuwa Muungano wa NASA, Bw Raila Odinga, na mgombea mwenzake wakati huo, Bw Kalonzo Musyoka, kama waliokwama kwenye mtindo wa mambo-zamani.

Ukiona mjadala huu ukiendelea wakati huu, miaka kumi baada ya kutolewa ahadi ya maendeleo ya kiteknolojia, basi unafahamu fika kwamba tulichezwa.

Maendeleo hayo yangekuwa yamepatikana kama, basi mjadala huu haungetokea wakati huu kwa kuwa mfumo huo ungekuwa umejaribiwa na kuthibitishwa unaaminika.Ni vigumu sana kwa watu kukubaliana kuhusu chochote wakati huu wa kampeni, lakini ili tulielewe vyema suala hili, yapo maswali mengi tunayopaswa kujibu.

Kuu zaidi: Je, sajili ya wapiga-kura ya kuthibitika, pamoja na mfumo wa kuhawilisha matokeo kutoka mashinani hadi ngazi ya kitaifa kwa usahihi, ni kwa manufaa ya nani? Ukijibu swali hilo kwa dhati ya moyo wako utajua tulipo.

Siku moja nikihariri habari za gazeti la Taifa Leo miaka kadha iliyopita, alirejea ofisini mwandishi fulani na pupa ya kuandika habari kuu kwenye gazeti huku akihemahema.

Aliiandika kwa fujo kweli, kisha akaiwasilisha kwangu ili niipitie, nikafanya hivyo upesi kwani muda ulikuwa umeyoyoma, na sikupenda kuchelewesha uchapishaji wa gazeti.

Baadaye, mhariri msimamizi akalalama kuwa ilikuwa na makosa chungu nzima. Tulilazimika kutafuta ukweli kwa kutumia teknolojia, kuhusu aliyeongeza mategu kwenye taarifa hiyo. Nahitmisha kwa kukwambia mwandishi alifedheheka kwa kutokuwa muungwana wa kukiri kosa lake. Mfumo ulimsemea.

Sasa turejee kwenye upigaji kura, tuambizane ukweli: mfumo wa kidijitali unaaminika zaidi kuliko sajili na fomu za kuchapishwa.

Wezi wa kura wanaweza kunaswa kwa njia rahisi iwapo watachakachua na kufuta majina ya watu, kutoa au kuongeza kura kutoka kapu hili hadi lile, na kadhalika. Hata hivyo, utendakazi wake unaishia hapo. Kenya ni mbuga mnamoishi watu! Siombi msamaha kwa kusema hivyo. Katika nchi ambako maagizo ya mahakama hayafuatwi, huna hakika na chochote. Mfumo wa kidijitali unaweza kuvurugwa, udanganyifu ukafanyika, ithibati kamili ikawepo, lakini bado serikali ikaamua kutotii sheria.

Hakikisho la haki na uwazi katika Uchaguzi Mkuu ujao lipo zaidi katika utashi wa serikali kuheshimu sheria.

mutua_muema@yahoo.com

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Adhabu kali dhidi ya msanii Kelly onyo kwa...

Cherotich, Wanyonyi wakata tiketi ya Riadha za Dunia U20...

T L