DOUGLAS MUTUA: Suluhu itafutwe kwa vita kati ya Israeli na Palestina

DOUGLAS MUTUA: Suluhu itafutwe kwa vita kati ya Israeli na Palestina

Na DOUGLAS MUTUA

VITA vinavyoendelea kati ya Israel na Palestina vimechochewa na uchu wa mamlaka wa mtu mmoja: Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin ‘Bibi’ Netanyahu.

Si siri kwamba Bw Netanyahu amedumu mamlakani kwa miaka 15 kwa ujanja wa kipekee wa kuweza kutumia hofu ya Waisraeli kwa manufaa yake ya kisiasa.

Usiichukulie sadfa kwamba vita hivyo – vinavyodaiwa kutokana na mzozo kuhusu mji mtakatifu wa Jerusalem – vimezuka wakati ambapo Netanyahu yumo hatarini ya kuondolewa mamlakani.Siku chache kabla ya vita vyenyewe kuzuka, Rais Reuven Rivlin wa Israel alimpa kiongozi wa upinzani, Bw Yair Lapid, jukumu la kuunda serikali ya muungano.

Hii ni baada ya taifa hilo kushindwa kupata waziri mkuu hata baada ya kufanya chaguzi nne tangu 2019.Inavyofanyika nchini Israel, ni lazima anayechaguliwa waziri mkuu awe na idadi kubwa ya wabunge ili aruhusiwe kuunda serikali.

Ikishindikana, rais anampa mmoja wa wawaniaji jukumu la kuunda serikali ya muungano wa kitaifa inayojumuisha vyama kadhaa.Katika chaguzi nne zilizofanyika tangu 2019, hakuna mwaniaji aliyefanikiwa kupata idadi ya wabunge inayohitajika.

Baada ya chaguzi tatu za kwanza, Rais Rivlin alimpa Bw Netanyahu fursa ya kuunda serikali lakini ‘Bibi’ akashindwa kuvisadikisha vyama vidogo kuungana naye, ndipo uchaguzi wa nne ukaandaliwa.

Hata baada ya uchaguzi wa nne, Rais Rivlin alimpa tena Bw Netanyahu fursa nyingine kuunda serikali lakini akashindwa.Badala ya kuandaa uchaguzi wa tano, Rais Rivlin alimpa kiongozi wa upinzani, Bw Lapid, fursa hiyo, shughuli anayoitekeleza unaposoma makala hii.

Uamuzi huo wa Rais Rivlin una maana kwamba Bw Lapid akifanikiwa, Bw Netanyahu ataondoka mamlakani, labda asalie tu kinara wa upinzani asipoamua kustaafu siasa.

Iwapo Bw Lapid hatafanikiwa, basi Rais Rivlin ataagiza uchaguzi wa tano tangu 2019 ufanyike. Hiyo ndiyo fursa pekee ya Bw Netanyahu kusalia mamlakani.

Bw Netanyahu hajawahi kukabiliwa na hatari kama hii, na si ajabu siku chache baada ya agizo la Rais, vikosi vya usalama vya serikali ya Netanyahu viliwachokoza Wapalestina kwenye Msikiti wa Al-Aqsa, Jerusalem, ndipo vita vikazuka.

Waziri Mkuu huyo anajua ilivyo vigumu kwa mtu yeyote kuunda serikali katika mazingira ya vita, hivyo, bila shaka, hiyo ni mbinu yake ya kulazimisha uchaguzi ufanyike.

Na kwa kuwa amedumu mamlakani kwa kuwatia hofu Waisraeli na kisha kujionyesha kama mlinzi na mtetezi wao, anatarajia kushinda uchaguzi ukifanyika wakati wa vita.

Bw Lapid, ambaye anajaribu kuunda serikali, ni mwanasiasa wa msimamo wa kadri anayeamini amani itapatikana Wapalestina wakiwa na taifa lao kando na Israel.

Bw Netanyahu, anayeshikilia msimamo mkali wa kuwakweza Waisraeli kuliko jamii nyingine za Mashariki ya Kati, ni mpenda vita anayesisitiza Wapalestina hawatawahi kuwa na taifa lao.

Wakati wa vita ambapo usalama wa Israel unahatarishwa, sera kama za Bw Netanyahu ndizo ambazo huwa maarufu zaidi. Kwa ufupi, vita vinavyoendelea ni kampeni ya Netanyahu kusalia mamlakani.

mutua_muema@yahoo.com

You can share this post!

BBI: Majaji watano walivyozima midundo ya Reggae

WANDERI KAMAU: Waliofanya KCSE wazingatie nidhamu kufaulu...