DOUGLAS MUTUA: Tamaa ya kutajirika haraka imevuruga sifa nzuri ya Kenya

DOUGLAS MUTUA: Tamaa ya kutajirika haraka imevuruga sifa nzuri ya Kenya

NA DOUGLAS MUTUA

HIVI Wakenya huwa na tatizo gani?

Imekuwaje kwamba hatuwezi kuwa na mtagusano na pesa za watu zikawafikia salama kama ilivyokusudiwa?

Mara zimeibwa Sh200 bilioni ambazo Serikali ya Kenya ilipaswa kutumia ili kukabiliana na athari za korona; mara serikali iliyoondoka juzi ilitumia karibu Sh50 bilioni siku zake za mwisho.

Na ukiuliza mafedha hayo yote yalifanyia nini, huonyeshwi.

Tumekuwa watu wa kuuza na kununua hewa, yaani huduma na bidhaa zisizokuwepo, ila pesa zinatoweka kikweli!

Ni utamaduni wa aina gani huu unaotukuza utapeli hivi kwamba ukiajiriwa katika idara ambayo inahusika na pesa, kisha ukose kuiba, unachukuliwa mjinga wa mwisho?

Habari kuu iliyotawala ndimi za wengi wakati huu inahusu Wakenya walioiba zaidi ya Sh30 bilioni nchini Marekani wakanunua majumba na magari ya kifahari kote duniani.

Pesa hizo zilitolewa na Serikali ya Marekani kwa ajili ya kuwanunulia chakula watoto walioathiriwa na janga la korona, lakini matapeli wetu waliamua watoto wakose lishe.

Ona sadfa inayojitokeza hapa: Huku Serikali ya Kenya ikiiba bila aibu pesa za kuwanunulia uji wagonjwa wa korona, Wakenya wadogo wanaoishi Marekani wanaiba za lishe ya watoto!

Tofauti ni kwamba papa waliohusika na ufisadi huo nchini Kenya wangali huru, tena wameficha mafedha hayo tusikojua, nao dagaa waliothubutu upumbavu huo Marekani wamenaswa.

Ninakutabiria hivi: walioiba nchini Kenya wataponea na kuendelea kufurahia mali yao ya wizi; waliotenda uhalifu huo Marekani watapokonywa kila kitu na kufungwa jela kwa muda mrefu.

Ikiwa una shaka na hili, uliza yaliyowatendekea jamaa za Akasha kutoka Mombasa waliokuwa wauzaji sugu wa mihadarati nchini Kenya kwa miongo mingi.

Baktash Akasha na Ibrahim Akasha walijipalia makaa walipothubutu kuuza bidhaa zao hizo Marekani; sasa kila mmoja anatumikia kifungo cha miaka 25 gerezani!

Je, unakumbuka ile ‘Sakata ya Kuku’ iliyohusisha hongo katika utoaji kandarasi za Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi (IIEC) yapata miaka 12 iliyopita?

Wakenya walioshukiwa kulipwa mamilioni ya pesa katika sakata hiyo ya uchapishaji wa karatasi za kupigia kura wangali huru, ila Waingereza waliowahonga walifungwa gerezani na kampuni zao zikafungwa!

Wakenya waliofungua akaunti za benki visiwani, vilivyo mbali na Kenya kisha wakaficha pesa za wizi huko au wakazitumia akaunti zenyewe kukwepa kulipa ushuru wangali huru.

Wahalifu kote duniani wanajua Kenya ni ‘Shamba la Wanyama’ ambako sheria zinatumiwa dhidi ya wanyonge pekee, hivyo anayetaka kutenda uhalifu wa pesa nyingi haoni ugumu wowote.

Kenya ni meza moja kubwa ambapo wahalifu hutakatishia pesa na kuwafanya watu wanaofanya kazi kwa bidii na uadilifu kuhisi kama wajinga wasiojua mbinu za kufaulu maishani.

Na kwa kuwa wahalifu hao wanaonekana kuendelea vizuri kimaisha, wametokea kuhusudiwa na watu wengi hivi kwamba tamaa ya kutajirika haraka imeongezeka mno.

Ni kwa sababu hii ambapo kumezuka vijana wanaojiita ‘waandishi wa mtandaoni’ ambao kwa hakika ni wadukuzi wanaojua kutumia teknolojia kuibia watu ili watajirike haraka.

Matokeo ya uhalifu wa ‘kutakatishia’ pesa Kenya ni kwamba mtu anayefanya kazi kwa bidii na kuhifadhi pesa zake ili angaa ajipange kimaisha anaambiwa pesa zake hazitoshi. Mbona?

Wanaotakatisha pesa wananunua ardhi na nyumba kwa pesa taslimu, tena kwa bei ya juu zaidi ili pesa hizo ziingie kwenye mfumo wa kifedha na kuwatoka mikononi haraka.

Hii ni changamoto kwa serikali mpya ya Kenya; mpango wa kiuchumi wa kuwainua watu wa kiwango cha chini utafaulu tu ikiwa uhalifu wa aina hii utakomeshwa mara moja. Kenya isiwe hema la kuwaficha wahalifu wa aina yoyote.

mutua_muema@yahoo.com

  • Tags

You can share this post!

Kebs yapiga marufuku aina 10 za mafuta ya kupikia nchini

TAHARIRI: Wakati wa serikali mpya kuinusuru soka ni sasa

T L