DOUGLAS MUTUA: Tanzania inahitaji katiba mpya, si hisani ya Rais

DOUGLAS MUTUA: Tanzania inahitaji katiba mpya, si hisani ya Rais

NA DOUGLAS MUTUA

NINAWAONEA imani ndugu zetu Watanzania ambao wanasherehekea kuondolewa marufuku ya mikutano ya kisiasa iliyowekwa na marehemu Rais John Magufuli mwaka wa 2016.

Mwendazake alichukua hatua hiyo mapema katika muhula wa kwanza wa utawala wake ili kudhibiti vyama vilivyopingana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) alichokuwa mwenyekiti wake.

Ijapokuwa marufuku ilitangazwa dhidi ya mikutano yote ya kisiasa, CCM iliendesha shughuli zake kama kawaida huku viongozi wa vyama vya upinzani wakikamatwa na kuzuiliwa.

Viongozi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, watetezi wa haki za binadamu, wanahabari na wengine waliodhaniwa kumpinga Magufuli walifungwa jela.

Baadhi ya watu walitoweshwa wasionekane tena mpaka leo, nayo miili ya watu walioteswa na kuuawa ikapatikana ikielea Bahari ya Hindi na Mto Rufiji.

Ilikuwa hatua ya kwanza ya kutekeleza mpango aliotangaza Magufuli mara tu baada ya kuanza kuiongoza nchi hiyo mwaka wa 2015: kuumaliza upinzani kabla ya kuondoka mamlakani.

Ni marufuku yaliyowezesha maovu hayo kuendelea ambayo mrithi wa Magufuli, Bi Samia Suluhu Hassan, ameondoa na kusababisha Watanzania kushangilia.

Nimesema ninawaonea imani Watanzania wanaosherehekea hatua hiyo kwa kuwa hawaonekani kujiuliza kwa nini Rais Samia amechelewa kutangaza hatua hiyo.

Kwamba tangazo hilo limetokea karibu miaka miwili baada ya Magufuli mwenyewe kukumbana na malaika wa kifo – mwezi Machi, mwaka 2021 – ni hali ya kutia wasiwasi.

Inaibua maswali mengi kuliko majibu: Kwa nini sasa? Ikiwa Bi Samia hakuyaunga mkono maovu hayo, kwa nini hakuondolea mbali marufuku hayo mara moja baada ya kuapishwa?

Kwa nini, katika enzi hii ya demokrasia na uhuru wa kujieleza, Rais Samia akiondoa marufuku hayo amewahimiza wanasiasa kufanya siasa safi kana kwamba ndiye mwelekezi wao?

Kwa maoni yangu, kiongozi huyo amewaruhusu wanasiasa kuandaa mikutano ya kisiasa kwa kuwa anajiandaa kutetea wadhifa wake miaka miwili ijayo. Na kwa kuwa amejituma sana kuisadikisha jamii ya kimataifa kwamba yeye ni tofauti na mtangulizi wake, Magufuli, ni lazima aonyeshe ishara kwamba anaheshimu haki za binadamu. Nimesema haki za binadamu, si Katiba ya Tanzania, kwa kuwa haki hizo zimekubaliwa kote duniani na yeyote asiyeziheshimu huchukuliwa kuwa nduli anayepaswa kutengwa.

Rais Samia hana budi ila kuigiza uwepo wa demokrasia na heshima kwa haki za binadamu ili pesa za misaada ziendelee kuingia, nalo jina la Tanzania litakate kimataifa.

Katiba ya Tanzania ilivyo sasa hivi inampa rais uwezo wa kufanya maovu mengi tu bila kuvunja sheria za nchi hata kidogo, ndiyo maana wanasiasa wa upinzani wanataka ibadilishwe.

Mwanzilishi wa taifa hilo, marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliwatabiria Watanzania kwamba angekuja kiongozi dhalimu aitumie kuwanyanyasa.

Utabiri huo ulitimia alipochaguliwa Magufuli na kuanza kuwadhulumu watu walio wapole na watulivu zaidi Afrika Mashariki na Kati.

Ukweli ni kwamba udikteta nchini Tanzania ni kitu kilichoidhinishwa kikatiba hivi kwamba taasisi ambazo zimejengwa na CCM kwa muda mrefu zinaweza kutumika kuuendeleza.

Usijiulize kwa nini kiongozi huyo ameruhusu mikutano ya kisiasa wakati ambapo anahitaji kudhibiti vyama vya upinzani zaidi ili ashinde uchaguzi ifikapo mwaka 2025. Yeye na CCM yake wanajua matokeo ya uchaguzi huo hata kabla ya kura kupigwa! Udhibiti ambao CCM inao katika taasisi zote za nchi hauwezi kuruhusu rais aliye mamlakani kushindwa na mpinzani yeyote.

Inasemekana barani Afrika, muhimu si wapigakura bali anayezihesabu kura zenyewe. Na upo katika hali nzuri ikiwa wewe ndiwe uliyemwajiri anayezihesabu kura.

Kimsingi, ikiwa kweli Rais Samia anataka kuwapa Watanzania uhuru wanaostahili na wala si kuwafanyia hisani, akubali Katiba ibadilishwe kabla ya uchaguzi mkuu wa 2025.

mutua_muema@yahoo.com

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali sasa idumishe juhudi zake kukabiliana na...

Gachagua achokoza nyuki akikamia kudhibiti Mlima

T L