DOUGLAS MUTUA: Tusije tukayazoea mauaji kama haya ya kusikitisha

DOUGLAS MUTUA: Tusije tukayazoea mauaji kama haya ya kusikitisha

Nina hofu kuu kwa kuwa Wakenya wameanza kuzoea mauaji yanayotekelezwa kila mara.

Siku hazipiti nyingi kabla ya kusikia mtu ameviziwa mtaani na kumiminiwa risasi mchana jua la utosi, akauawa papo hapo, nao wauaji wakaingia mitini wasipatikane kamwe.

Ukiwa makini utatambua kuwa maelezo kuhusu maisha ya wahanga wa mauaji hayo yanafanana: waliishi maisha ya siri; walikuwa na mafedha yasiyoisha; walikoyatoa mafedha yenyewe hakujulikani; dalili zinaonyesha walikuwa wahalifu sugu.

Maelezo hayo yanapotolewa, tunaonekana kusadiki kwamba marehemu walikuwa wahalifu, tunasahau kuwa watu hao wameuawa kinyume cha sheria, yaani na wahalifu.

Tunaporejea kwenye shughuli zetu na kupuuza itakavyokuwa hatima ya tukio la mauaji, tunawapa ujasiri wahalifu hao kutafuta watu wengine wa kutesa na kuua. Kwa namna fulani tunakubali kwamba mchakato wa sheria si muhimu; polisi wanaweza kuwaua washukiwa, nasi tukikosana tunaweza kulana maini tutakavyo bila kuadhibiwa.

Hofu yangu inatokana na ukweli kuwa mauaji ya aina hii nchini Kenya hayajatokea mara moja pekee na kila mara tunawashuku wahalifu na vikosi maalumu vya polisi. Nilikuwa nchini Kenya mapema miaka ya 2,000, kundi haramu la Munguki likiwahangaisha na kuwaangamiza kwa kuwakata shingo wanachama wake waliodaiwa kulisaliti.

Ghafla ulizuka mtindo wa wahalifu wengine kuwaua watu kwa mtindo huo, na kila mara tuliamini kwamba ni maluuni wa Mungiki waliokuwa wakiangamizana.

Wanahabari wapekuzi walikuwa na taarifa kwamba kikosi maalum cha polisi, Kwekwe, kilichoundwa kwa ajili ya kuangamiza Mungiki, kiliwaua washukiwa kwa mbinu hizo-hizo.

Ilidaiwa kuwa wahalifu, wake kwa waume, wangekamatwa na kulazimishwa kufanya ngono wenyewe kwa wenyewe, kisha kuuawa kinyama na miili yao kukatwakatwa kwa mtindo wa Mungiki.

Raia waliposikia eti wanawake walioshukiwa kuwa wanachama wa Mungiki walibakwa na kuuawa, waliamini unyama huo wote ulitendwa na wahalifu. Polisi hawakuhusika eti.

Vipo visa ambapo polisi waliwapiga risasi na kuwajeruhi washukiwa, wakawapeleka hospitalini, baadaye Kwekwe wakafika na kuwatoa humo bila idhini na kisha kuwaua.

Kutokana na mazoea ya Wakenya kwamba haidhuru kwa washukiwa kuuawa kabla ya kufikishwa mahakamani, hata kisa cha aliyekuwa mahabusu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wakili Paul Gicheru, kitapuuziliwa mbali.

Bw Gicheru, aliyeshtakiwa na ICC kwa tuhuma za kuwahonga na kuwashawishi watu walionuia kutoa Ushahidi dhidi ya Rais Willaim Ruto aliposhtakiwa katika mahama hiyo ya Uholanzi, alifariki hivi majuzi katika hali isiyoeleweka vyema.

Nimewasikia watu ambao, badala ya kuulizana ni akina nani walionuia kumuua wakili huyo aliyejisalimisha kwa ICC, wanampuuzilia mbali kuwa mhalifu aliyeonjeshwa shubiri yake.

Maoni kama hayo yalitolewa mwaka jana pale watu walioshukiwa kuwa wahalifu walipokamatwa mjini Kitengela kisha miili yao ikapatikana ikielea kwenye mito mbalimbali.

Tatizo la kuwa na mtizamo kama huo ni kwamba jamii haitafakari kuhusu hatari inayoikabili; wauaji wasipokomeshwa hubaki miongoni mwetu, hivyo hatuko salama.

Ni sharti tubuni utamaduni wa kuhimiza umuhimu wa kufuata sheria kikamilifu, wahalifu wauawe tu ikiwa mahakama itawahukumu kifo. Vinginevyo, tunajichongea wenyewe.

mutua_muema@yahoo.com

  • Tags

You can share this post!

Gavana Nassir kuimarisha idara kukabili majanga

Jaji afungulia wanasiasa wasio na digrii kuwania ugavana

T L