DOUGLAS MUTUA: Uchina isipime corona kwa njia ya kudhalilisha

DOUGLAS MUTUA: Uchina isipime corona kwa njia ya kudhalilisha

Na DOUGLAS MUTUA

UCHINA, taifa ambako janga la corona lilianzia, limezuka na mengine! Watu mitandaoni wamechukizwa mno; wanasema ugumu wa maisha ulioletwa na corona unatosha, hawataki kunyanyaswa.

Sasa watu wanaoingia taifa hilo kutoka nje wanafanyiwa vipimo vya corona kwa njia ya kuwavunjia heshima.

Mataifa kadhaa yamelalamika kwamba raia wake wakitaka kuingia Uchina wanalazimishwa kupimwa ugonjwa huo kwa kutolewa sampuli upande wa nyuma.

Ni kutokana na malalamiko hayo ambapo Japan imeiandikia serikali ya Uchina na kuiagiza isithubutu kuwagusa Wajapan makalioni, itumie njia za kawaida zilizokubalika duniani.

Kawaida ukitaka kupimwa corona, sampuli ya ukamasi au kikohozi hutolewa puani na kooni mtawalia, shughuli ambayo watu hawaipingi japo pia inaumiza kidogo.

Hiyo ya watu kupimwa kutokea makalioni imetokea kupingwa vikali kwa sababu inakwenda kinyume na maadili ya watu wengi duniani.

Malalamiko ya kwanza kuihusu yalitolewa mwezi jana na wanadiplomasia wa Marekani wanaofanya kazi Uchina.

Walisema wanalazimishwa kutolewa sampuli huko, kitu wanachochukulia kuwa ubaguzi na uvunjaji wa heshima zao.

Ripoti nyingine zilisema kuwa mtu yeyote anayefika nchini humo, hata ikiwa hajatokea eneo lililo na wagonjwa wengi wa corona, anapimwa kwa njia hiyo chukizi bila hiari yake.

Ijapokuwa Uchina ilisema haikuwapima Wamarekani waliolalamika kwa njia hiyo isiyopendeza, ilisema ndiyo njia muafaka zaidi.

Serikali ya Uchina ilisema watu wanahitaji kupimwa corona kwa kutolewa sampuli sehemu ya nyuma kwa sababu virusi hivyo vinaaminika kukaa mwilini kwa muda mrefu hata ikiwa mgonjwa hana dalili.

Ilieleza kwamba itaendelea kutumia njia nyingine zilizokubaliwa kwa sababu hiyo ya makalioni inachosha na inawachukua wataalamu muda mrefu kuikamilisha.

Lakini kumbuka Uchina ni ile-ile, haiaminiki tangu hapo! Corona ilipozuka ilificha kabisa, daktari aliyefichua kuzuka kwa ugonjwa huo akatiwa kizuizini na hatimaye akafariki.

Na inaaminika Uchina imeficha kabisa takwimu sahihi za raia wake ambao wamefariki kutokana na ugonjwa huo hivi kwamba mpaka sasa dunia haijui ni wangapi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limelalamika kuhusu ukora wa Mchina katika kukoroga takwimu na kutoa zisizo sahihi ili taifa hilo lionekane limekabiliana na janga hilo vilivyo.

Vilevile, Uchina inajulikana kwa kukiuka haki za binadamu, ikiwepo kuwaua Waislamu, watetezi wa demokrasia na kuwatumia wafungwa kama watumwa.

Licha ya Marekani na mataifa mengine kulalamika kuhusu maovu hayo, Uchina haijachukua hatua yoyote kubadili mambo. Imejipa hamnazo na kuzidisha maovu.

Ni kutokana na uovu huo ambapo watu wengi wanaamini kwamba Uchina inaweza kufanya chochote kisha itumie nguvu na ushawishi wake duniani kukabiliana na shutuma hizo. Tayari watu wengi wameapa kutotia guu Uchina hata kwa shughuli rasmi kwa sababu hawataki vipimo vya kulazimishiwa.

Njia hiyo ya kutolewa sampuli kwa kuingiliwa nyuma hutumika kote duniani ili kuwapima wanaume ugonjwa wa tezi dume, hatua ambayo imewafanya wengi kususia shughuli hiyo.

mutua_muema@yahoo.com

You can share this post!

DINI: Tuwe kama bundi; tuutumie usiku ‘kuona’ yale...

JAMVI: Hofu jahazi la Ruto limeanza kupasua nyufa Mlima...